Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuweka kando tofauti zao na kushikamana kwa ajili ya kuhakikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika Ofisi za INEC Manispaa ya Iringa, kufuatia uteuzi wake uliofanywa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ngajilo amesisitiza kuwa mshikamano na kuvunjwa kwa makundi ya ndani ya chama ni msingi imara wa ushindi wa CCM.
“Nawaomba wanachama wenzangu tuweke mbele maslahi ya chama. Tuvunje makundi, tushikamane kama familia moja ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM hapa Iringa Mjini,” amesema Ngajilo.
Ngajilo ameeleza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Iringa Mjini kwa uadilifu, uwazi na kushirikiana nao katika kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Aidha, amewataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika mchakato wa uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika kutumia haki yao ya kidemokrasia.
Fadhili Ngajilo ni miongoni mwa wagombea walioteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika octoba mwaka huu