Chama cha ACT Wazalendo kimepinga kwa ukali hatua ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumzuia mgombea wake wa urais, Luhaga Joelson Mpina, kurejesha fomu za uteuzi, kikieleza kuwa maamuzi hayo ni ‘ya aibu, kinyume cha Katiba na hatari kwa demokrasia ya nchi’.
Katika barua ya tarehe 27 Agosti 2025 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, ACT Wazalendo kimeeleza kushangazwa na maelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi kupitia barua ya tarehe 26 Agosti 2025, kwamba Mpina asifike ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi kwa kisingizio cha kupokea nakala ya barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotengua uteuzi wake.
“Maamuzi haya sio tu kwamba ni ya aibu bali yanaibua maswali mengi juu ya uadilifu, umakini, uweledi na uhuru wa Tume ambayo imepewa dhamana ya kikatiba kuwa huru katika kusimamia Katiba, Sheria, Kanuni na utaratibu unaongoza usimamizi wa Uchaguzi nchini”, amesema Shaibu.
Shaibu ameikumbusha INEC kuwa Mpina alipewa fomu tarehe 15 Agosti 2025 baada ya kukidhi vigezo vya kisheria, ikiwemo kupata wadhamini, kujaza fomu na kuhakikiwa, hivyo Tume haina mamlaka ya kikatiba wala kisheria kumzuia mgombea kurejesha fomu hizo.
“Sheria haitoi nafasi kwa Tume kukataa kupokea fomu au kutomteua Mgombea isipokuwa kwa njia ya Pingamizi linalowekwa dhidi ya Mgombea kwa utaratibu uliopo chini ya Kifungu cha 36 na 37 cha Sheria na Kanuni ya 22 ya Kanuni za Uchaguzi (2025). Kwa maana nyengine hakuna kifungu chochote cha Sheria, Katiba au Kanuni kinachotoa Mamlaka kwa Tume kuzuia Mgombea asirudishe fomu iliyotolewa na Tume baada ya kukidhi vigezo vya uchukuaji wa fomu”, ameongeza Shaibu.
Chama hicho kimeitaka INEC kufuta barua ya tarehe 26 Agosti 2025 na kuruhusu Mpina kurejesha fomu kama ilivyopangwa awali, kinyume chake hatua hiyo itathibitisha kwa umma kuwa Tume “sio huru, haiwezi kutenda haki na imekuwa chombo cha kisiasa.”
“Tume inajua au ilipaswa kujua kuwa Msajili anayo nafasi ya kumuwekea Mgombea pingamizi katika siku iliyopangwa kwa ajili ya uteuzi na baada ya kusikiliza upande wa Mgombea juu ya pingamizi zilizowekwa kwa wakati maalum kama inavyoelekezwa na Kifungu cha 37 na sio kwa Tume kufanya maamuzi baada ya kupokea amri na maelekezo kupitia nakala ya barua ya msajili”, ameeleza.
ACT Wazalendo imesisitiza kuwa inatarajia hatua za haraka kutoka INEC ili kurejesha uhalali wa mchakato na kulinda misingi ya Katiba, demokrasia na utawala bora.