Latest Posts

MAFANIKIO YA SEKTA YA NYUMBA KATIKA AWAMU YA SITA YA DKT SAMIA: UONGOZI WA KUSUKUMA MAGEUZI

Katika kipindi cha miaka minne tu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya nyumba imepata upepo mpya wa maendeleo unaoweza kufananishwa na mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Kupitia Shirika la Nyumba la Taifa, nchi yetu imejionea mabadiliko makubwa katika ujenzi wa nyumba, majengo ya biashara, ukamilishaji wa miradi mikubwa iliyokwama, utekelezaji wa sera ya ubia, na uboreshaji wa mapato ya Shirika.

Ni simulizi linalodhihirisha kwamba kwa uongozi makini, taasisi za umma zinaweza kugeuka injini za ukuaji, chanzo cha matumaini kwa wananchi na mfano wa kuigwa katika usimamizi wa miradi mikubwa ya kimkakati.

Ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya nyumba ndiyo moyo wa maendeleo ya jamii yoyote. Nyumba bora siyo anasa, ni heshima ya binadamu. Nyumba bora siyo fahari binafsi, ni ulinzi wa familia, ni nguzo ya ustawi, ni ngome ya uchumi wa kaya na taifa. Kwa kufahamu ukweli huu, Rais Samia ameweka nguvu kubwa kuhakikisha NHC inafanya kazi kwa kiwango cha juu na kugeuka chombo cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

Miradi Iliyokwama yafufuliwa Upya

Katika miaka kadhaa, tulishuhudia miradi kadhaa mikubwa ikikwama, majengo yakisimama kama alama za kukata tamaa, na matarajio ya wananchi kuyeyuka taratibu. Hata hivyo, kwa hatua thabiti zilizochukuliwa na Rais Samia, miradi hiyo imerejeshwa kwenye mstari wa utekelezaji. Morocco Square ni mfano hai: mradi uliosimama tangu 2018 leo umekamilika kwa asilimia 100 na umekuwa kitovu cha biashara na makazi jijini Dar es Salaam.

Sasa Morocco Square si jengo tu – ni ishara ya kujiamini, ni kioo cha jinsi Tanzania inaweza kusimama tena hata pale palipokuwa na changamoto. Sehemu za biashara zimepangishwa kwa asilimia 100, ofisi kwa asilimia 95, na hoteli yenye vyumba 81 sasa inafanya kazi kwa kiwango cha juu. Kati ya nyumba 100 za makazi, tayari 98 zimeuzwa, na mauzo ya nyumba chache zilizobaki yanaendelea kwa kasi.

Vivyo hivyo, mradi mkubwa wa Kawe 711 umeendelea kufufuliwa na sasa ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 70, ukitarajiwa kukamilika mwaka 2026. Mradi huu wenye thamani ya shilingi bilioni 169 siyo tu makazi ya kisasa yenye nyumba 422, bali pia unajumuisha sehemu za biashara zinazotarajiwa kuongeza mzunguko wa uchumi wa jijini Dar es Salaam. Mradi huu ukikamilika, utakuwa mfano wa dhahiri wa namna uthubutu wa kisera unavyoweza kugeuza changamoto kuwa fursa.

Samia Housing Scheme – Ndoto Inayogeuka Uhalisia

Samia Housing Scheme, mradi wenye nyumba 5,000, umeleta upepo mpya wa matumaini. Huu ni mradi unaobeba jina la Rais Samia kwa sababu unataka kuacha alama isiyofutika katika sekta ya nyumba nchini. Katika Kawe, nyumba 560 zimekamilika kwa asilimia 100, na zote ziliuzwa hata kabla ya mradi kumalizika. Wanunuzi tayari wameanza kukabidhiwa funguo na kuhamia katika nyumba zao mpya. Hii ni dalili kwamba wananchi wana imani kubwa na miradi ya NHC.

Katika Dodoma, nyumba 160 zimeanza kujengwa eneo la Medeli, zikijibu moja kwa moja ongezeko la mahitaji ya makazi katika Makao Makuu ya nchi. Dodoma, ambayo imekuwa na ongezeko kubwa la wakazi kutokana na Serikali kuhamishia shughuli zake kuu, sasa inapata makazi ya kisasa yanayolingana na hadhi yake. Vilevile, nyumba 260 zinajengwa Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam, na maandalizi ya nyumba 500 nyingine Kawe yanaendelea.

Kwa uchambuzi wa kina, Samia Housing Scheme ni zaidi ya ujenzi wa nyumba. Ni suluhisho la changamoto ya makazi kwa wananchi wa kipato cha kati na cha chini. Ni mkakati wa kupunguza pengo la mahitaji ya nyumba nchini, ambalo limekuwa kubwa kwa miaka mingi. Ni mpango wa kutoa ajira kwa maelfu ya vijana katika sekta ya ujenzi, biashara ya vifaa na huduma nyingine zinazohusiana. Ni mradi wa kijamii, kiuchumi na kimaendeleo kwa pamoja.

Mageuzi ya Mandhari ya Miji Yetu

Mbali na miradi ya makazi, NHC imewekeza katika majengo ya biashara ya kisasa kote nchini. Morogoro sasa inajenga Uluguru Plaza, hatua ya awali ikiwa imekamilika kwa 30%, lakini matarajio ni makubwa kwamba jengo hili litaongeza thamani ya kiuchumi ya mji huo. Tanga inashuhudia ujenzi wa Mkwakwani Plaza, Tabora inaona mwanga mpya kupitia Tabora Commercial Complex, na Iringa pia inaanza kuandika historia yake kwa Iringa Commercial Complex.

Masasi Plaza mkoani Mtwara umefikia asilimia 75, Mtanda Commercial Building Lindi umefikia asilimia 75, na 2H Commercial Building Morogoro sasa uko katika hatua ya mwisho kwa asilimia 90. Singida imepata jengo jipya la 2F Plaza ambalo lipo hatua za ujenzi, na Arusha inajenga Meru Plaza litakaloongeza heshima ya jiji la kitalii. Bukoba inajenga Kashozi Business Center, na Mtwara maghala ya kuhifadhia mazao yanaendelea kujengwa ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Kwa uchambuzi wa kimkakati, hii ni hatua ya makusudi ya kuhakikisha kila mkoa unapata alama ya maendeleo. Majengo haya hayataongeza mapato ya biashara pekee, bali yataongeza thamani ya ardhi, yataboresha taswira ya miji, na kuvutia wawekezaji wapya.

Athari za Moja kwa Moja kwa Taifa

Miradi hii ina athari kubwa kwa taifa. Kwanza, inaongeza ajira. Kwa kila jengo linalojengwa, mamia ya vijana wanapata ajira za moja kwa moja kama mafundi, wahandisi, wasanifu, na maelfu ya wengine wanapata ajira zisizo za moja kwa moja kupitia biashara ndogondogo zinazohusiana na ujenzi. Pili, inapanua mapato ya Serikali kupitia kodi. Kila nyumba, kila ofisi, kila duka linapokamilika, linaongeza chanzo cha kodi ya mapato, kodi ya majengo, na kodi ya biashara. Tatu, inaboresha maisha ya wananchi kwa kuwapa makazi bora na salama, na mazingira ya biashara yenye hadhi.

Hivyo basi, mafanikio haya hayapimwi tu kwa idadi ya nyumba zilizojengwa, bali pia kwa athari zake za kijamii na kiuchumi.

NHC Kama Injini ya Uchumi

Mafanikio makubwa ya kifedha ya Shirika yanaonyesha taswira ya taasisi imara inayosimamiwa kwa weledi. Makusanyo ya kodi yameongezeka kutoka bilioni 7.5 mwaka 2021 hadi bilioni 9.4 mwaka 2025. Gawio kwa Serikali kimeongezeka mara tano, kutoka bilioni 1 mwaka uliopita hadi bilioni 5.5 mwaka 2025. Rasilimali za Shirika nazo zimepanda kutoka trilioni 5.04 mwaka 2021 hadi trilioni 5.47 mwaka 2024.

Takwimu hizi zinaonyesha kwamba NHC haifanyi kazi kwa nadharia tu, bali inatoa matokeo ya moja kwa moja. Kwa kila mradi unaokamilika, kuna ongezeko la rasilimali, ongezeko la mapato, na ongezeko la uwekezaji mpya.

Ubia Unaobadilisha Taswira ya Miji

Sera ya ubia iliyohuishwa mwaka 2022 imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma. Tayari miradi 21 yenye thamani ya bilioni 179 imesainiwa, na miradi 18 ipo kwenye utekelezaji wa moja kwa moja. Miradi 61 mingine yenye thamani ya zaidi ya bilioni 600 ipo katika hatua za uhakiki wa mwisho kabla ya utekelezaji.

Kwa mfano, eneo la Kariakoo pekee, nyumba 172 zilizokuwa za zamani zitabadilishwa na zaidi ya nyumba 2,100 za kisasa, zikiwa na nafasi za biashara na makazi. Mageuzi haya hayawezi kupuuzwa: ni mfano wa jinsi ubia sahihi unavyoweza kubadilisha mandhari ya miji na kuongeza tija ya uchumi.

Utekelezaji wa miradi hii una manufaa makubwa ikiwemo kuongeza upatikanaji wa nyumba bora za makazi na biashara, kuongezeka kwa ajira kwa watanzania na kupendezesha mandhari ya miji yetu na wigo wa kodi na mapato ya Serikali.

NHC imeendelea kufanya vikao kadhaa na wapangaji wa eneo la Kariakoo na Upanga na wapangaji wamepisha wabia kufanya uendelezaji unaokusudiwa. Wapangaji waliokuwa wanalipa kodi vizuri wamehakikishiwa kurejeshewa upangaji wao pindi ujenzi wa majengo mapya utakapokamilika.

Katika kuhakikisha miradi ya Ubia inatekelezwa kwa uhakika na kuwa na ubora na imara, unaokubalika, Shirika limeunda timu ya Wataalamu wa fani zote za ujenzi ambao wanafuatilia kila hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Siyo hivyo tu, bali NHC imekuwa ikiendelea kupanua wigo wa shughuli zake kwa kutumia teknolojia za kisasa na utaalamu wa ndani, ili kuwezesha uanzishaji wa miradi mipya ya makazi, kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa, likiwamo na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), kutekeleza miradi ya ukandarasi, ujenzi wa vitega uchumi, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa miradi mbalimbali nchini na kutekeleza sera ya ubia.

Kimsingi kwamiaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, NHC limepiga hatua kubwa katika kuboresha sekta ya nyumba nchini. Mafanikio hayo yanadhihirisha dhamira ya Serikali kuimarisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya makazi bora. Kwa mipango madhubuti, NHC itaendelea kuwa mwanga wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

Changamoto Zilizopo na Mikakati ya Suluhisho

Bado zipo changamoto. Wadaiwa sugu wa kodi ya pango wamekuwa tatizo kubwa, ucheleweshaji wa malipo ya miradi ya Serikali umesababisha kusuasua kwa baadhi ya miradi, na riba kubwa za mikopo bado ni changamoto. Hata hivyo, Shirika limechukua hatua madhubuti: kuvunja mikataba ya wapangaji wasiolipa, kuanzisha amana za pango kwa wapangaji wapya, kushirikiana na Credit Reference Bureau kudhibiti wadaiwa, na kushauri Serikali kupunguza VAT kwa nyumba za gharama nafuu na riba za mikopo hadi chini ya asilimia 10.

Mustakabali wa Sekta ya Nyumba

Maandalizi ya kuzindua hati fungani ya Nyumbani Bond yanaendelea, hatua itakayowezesha wananchi na taasisi kuwekeza moja kwa moja katika ujenzi wa nyumba. Kupitia njia hii, wananchi watahusika moja kwa moja katika maendeleo ya sekta ya nyumba, siyo kama wanunuzi pekee bali pia kama wawekezaji. Hatua hii itakuwa chachu ya kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kupunguza tatizo la makazi nchini.

Urithi wa Kihistoria

Kwa kuangalia muktadha wote huu, ni wazi kwamba mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kifupi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia yanathibitisha ukweli mmoja muhimu: sekta ya nyumba inaweza kuwa injini ya uchumi na chanzo cha heshima ya taifa. Kila jengo linalosimama ni alama ya mageuzi yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Kila familia inayopokea funguo za nyumba mpya ni simulizi la matumaini. Kila mji unaojipatia jengo jipya la biashara ni mlango mpya wa ajira na mapato. Rais Samia ameweka msingi wa urithi wa kihistoria, urithi ambao vizazi vijavyo vitaukumbuka kama zama ambazo Tanzania ilibadilisha sura ya makazi yake na kujenga mustakabali mpya wa taifa lenye heshima na utu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!