Vyombo vya usalama mkoani Tabora vinamshikilia kijana mmoja kwa tuhuma za kuandika ujumbe wa uchochezi kwenye kuta za nyumba za watu wilayani Urambo, ukihamasisha wananchi kutoshiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Ujumbe huo uliokuwa umeandikwa kwenye baadhi ya kuta unasomeka: “Usiende kupiga kura, nenda kwenye maandamano tarehe 29.”
Akizungumza na wanahabari leo, Oktoba 17, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, Paul Chacha, amesema kijana huyo amekamatwa na anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo vimejipanga kikamilifu kuhakikisha hali ya utulivu inabaki kuwa thabiti katika kipindi chote cha kuelekea na wakati wa uchaguzi.
Ameongeza kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayejihusisha na uandishi wa ujumbe au vitendo vinavyohamasisha vurugu, maandamano haramu, au ushawishi wa kisiasa unaolenga kuvuruga amani ya uchaguzi.
Aidha, RC Chacha amewatoa hofu wamiliki wa vituo vya mafuta mkoani humo kufuatia uvumi uliosambaa kwamba vituo hivyo vinaweza kushambuliwa au kuchomwa moto siku ya uchaguzi, akiwahakikishia kuwa ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote muhimu.