Latest Posts

LEMA ASEMA MAISHA YAKE YAPO HATARINI, POLISI WAANZA UFUATILIAJI

Jeshi la Polisi Tanzania limetoa kauli kutokana na taarifa zilizotolewa na mwanasiasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, kupitia mitandao ya kijamii, akidai kuwa usalama wake upo hatarini.

Kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 17, 2025 kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, Msemaji wa Jeshi hilo DCP David Misime amesema jeshi linafuatilia kwa karibu taarifa hizo huku likimtaka Lema kufika kituo cha polisi ili kutoa maelezo rasmi kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

“Tunamsisitiza afike katika Kituo cha Polisi ili awasilishe taarifa yake hiyo rasmi kwa hatua zingine kwani ndiyo utaratibu wa kisheria”, imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya Lema kuandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram, akiomba ulinzi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akidai kuna watu wanaomfuatilia na kuhofia kuwa wanaweza kumdhuru.

“Mheshimiwa Rais, maisha yangu yako katika hatari kubwa. Tafadhali, naomba kwa unyenyekevu mkubwa unisikilize. Kwa sasa, kuna watu ambao wananifuatilia kwa karibu sana. Hata jioni ya leo, wameonekana maeneo ya nyumbani kwangu, na nina hofu kwamba wangeweza hata kumdhuru mtu yeyote ambaye si mimi,” aliandika Lema.

Aidha, mwanasiasa huyo aliongeza kuwa kutokana na hofu hiyo, anaona ni bora awekwe mahabusu kwa hiari hadi kipindi cha uchaguzi kipite ili kulinda usalama wake na wa familia yake.

Jeshi la Polisi limetoa wito na kusisitiza kwa baadhi ya viongozi na wananchi kuendelea kuzingatia utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha taarifa sahihi kwa jamii na mamlaka za haki jinai ili kuepusha kile ilichokiita upotoshaji na taharuki zisizo za lazima.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!