Serikali ya Tanzania imeiomba Marekani kuondoa vikwazo vya viza kwa Watanzania wanaosafiri kwenda nchini humo, pamoja na vikwazo vingine vya kiuchumi na kiusafiri vilivyowekwa dhidi ya Tanzania, ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wananchi wa nchi hizo mbili.
Ombi hilo limewasilishwa wakati wa mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, pamoja na ujumbe maalum wa wajumbe 11 wa Baraza la Wawakilishi la Marekani (Congress) kutoka vyama vyote viwili vikuu nchini humo.

Kikao hicho cha ngazi ya juu kilichofanyika Julai 27, 2026, katika Ofisi za zamani za Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Ngome), Upanga jijini Dar es Salaam, kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Huduma za Kijeshi, Ulinzi na Usalama ya Baraza la Wawakilishi la Marekani, Ronny Jackson.
Pamoja na kuwasilisha ombi hilo la kuondoa vikwazo, pande hizo mbili zilijadili maeneo ya kipaumbele ikiwemo fursa za biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama, pamoja na amani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Ujumbe wa Marekani uliipongeza sana Tanzania kwa mchango wake katika kudumisha amani na usalama wa kikanda, ikiwemo juhudi za kupambana na ugaidi na ushiriki katika operesheni za kulinda amani barani Afrika.
Aidha, pande hizo mbili zilikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika maeneo yenye maslahi ya pamoja na pia kukubali kupitia tena maombi yote ya vikwazo yaliyowasilishwa rasmi na Tanzania na kukubaliana kukutana tena katika vikao vijavyo vitakavyofuata kwa lengo la ufuatiliaji kati ya nchi mbili.