Watu nane wamepoteza maisha huku wengine 66 wakijeruhiwa kutokana na ajali iliyohusisha mabasi mawili ya abiria yaliyokuwa yakisafiri kwenda mikoani, yaliyogongana uso kwa uso katika Kijiji cha Ibiwa, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, majira ya saa 12:00 asubuhi, Agosti 2, 2026.
Ajali hiyo imehusisha basi la kampuni ya Isamilo lenye namba za usajili T 428 EPX na basi la kampuni ya Libanika lenye namba za usajili T 897. Kati ya majeruhi 66, watu tisa wameripotiwa kuwa katika hali mbaya na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Wakizungumza wakiwa hospitalini, baadhi ya majeruhi wamedai kuwa chanzo cha ajali hiyo kilikuwa ni mwendo kasi wa moja ya mabasi hayo. Wamedai kuwa dereva wa basi moja alijaribu kulipita lori lililokuwa mbele yake, lakini katika jitihada za kulikwepa alijikuta akigongana uso kwa uso na basi lililokuwa likitokea upande wa pili wa barabara.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amewataka madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuacha uzembe pamoja na mwendo kasi, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza ajali zisizo za lazima zinazogharimu maisha ya wananchi na kusababisha majeraha makubwa.
