Asnat Hamisi, mkazi wa Kijiji cha Msangamkuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, ameiomba jamii kujitokeza kumsaidia mtoto anayefahamika kwa jina la Alkamu, mwenye changamoto ya kichwa kikubwa.
Asnat amesema hali ngumu ya maisha imemfanya ashindwe kumudu gharama za matibabu ya mtoto huyo mwenye umri wa miaka 10, ambaye anahitaji matibabu yenye gharama ya takribani shilingi milioni mbili (2,000,000).

Mama huyo ametoa wito huo mara baada ya kupokea msaada wa chakula cha mtoto, unga wa lishe na mahitaji mengine kutoka kwa kikundi cha Dadaz Mtwara DC, ambacho kinaundwa na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Aidha, kikundi hicho pia kimetoa msaada wa kiti mwendo kwa mtoto anayefahamika kwa jina la Yazidu, mwenye changamoto ya uti wa mgongo, ili kumwezesha kuhudhuria shule kwa urahisi.

Asha Issa, mama mzazi wa Yazidu amesema kupatikana kwa kiti hicho kutarahisisha kwa kiasi kikubwa ushiriki wa mwanawe katika masomo, kwani hapo awali alikuwa anashindwa kukaa muda mrefu na kutumia muda mwingi akiwa amelala kutokana na hali yake.
“Namshukuru Mungu na kikundi cha Dadaz Mtwara DC kwa msaada huu. Nitahakikisha namwandikisha mtoto shule kwani sasa anaweza kukaa kupitia kiti hiki.”Amesema Asha.
Hivyo ukiwa kama mwana jamii unaweza kuchangia chochote ulichojaaliwa ili kuwezesha ghalama za matibabu kwa mtoto Alkamu kupitia namba ya simu ya mama ake Alkamu anaefahamika kwa jina la Asnat Hamisi 0688059549