Latest Posts

KAMATI YA FEDHA GEITA DC YABANA WASIMAMIZI WA MIRADI

Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita,  imefanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Geita.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Butobela, Mhe. Pascal Mapung’o, amewataka Wahandisi wa Halmashauri kuhakikisha wanashughulikia kwa wakati kasoro zote zinazoonekana kwenye miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutumika.

“Kasoro zote tulizoziona kwenye miradi zifanyiwe kazi mapema ili miradi ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Mhe. Mapung’o.

Aidha, amewataka wasimamizi wa miradi kuzingatia kikamilifu maelekezo yanayotolewa na Halmashauri pamoja na kuzingatia gharama zilizopangwa kwa kila mradi ili kuepuka matumizi yasiyo na tija.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chigunga, Mhe. Anthony Anacretia, ametoa wito kwa viongozi wa kata na vijiji kuendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, hususan katika maeneo yanapotekelezwa miradi.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi. Sarah Yohana, ambaye pia ni Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, amewataka mafundi ujenzi kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ili ikamilike kwa wakati uliopangwa.

“Ninawasihi mafundi kuongeza kasi ya ujenzi, huku wasimamizi wa miradi wakihakikisha mafundi wanalipwa kwa wakati,” amesema Bi. Sarah.

Vilevile, Bi. Sarah amewataka wasimamizi wa miradi kuwashirikisha wananchi waliopo katika maeneo ya utekelezaji wa miradi na kuwapa taarifa pindi fedha za miradi zinapoingia ili wananchi washiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo.

Kamati hiyo, ikijumuisha wataalam kutoka Halmashauri, imetembelea miradi ya ujenzi wa shule, ukarabati wa miundombinu ya madarasa, ujenzi wa nyumba za watumishi pamoja na ununuzi wa vifaa katika nyumba hizo. Thamani ya miradi hiyo ni Shilingi Bilioni 2.1.

Miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha kutoka vyanzo mbalimbali vikiwemo Mapato ya Ndani ya Halmashauri, BOOST pamoja na mchango wa Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu ya Geita kwa jamii (CSR–GGML).

Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Pia imewapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa jitihada zao za kuleta maendeleo kwa wananchi wa Geita.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!