Latest Posts

DKT KIJAJI: FANYENI TATHMINI NA KUSIMAMIA IPASAVYO MAENEO YA UHIFADHI KUMALIZA MIGONGANO KATI YA BINADAMU NA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

 

Bodi ya Menejimenti ya Taasisi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetakiwa kufanya tathmini ya kina na kuimarisha usimamizi wa Wanyamapori ili kupunguza na kuzuia athari zitokanazo na migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu.

Maelekezo hayo yametolewa Julai 7,2026 Mkoani Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Menejimenti ya TAWA.

Pia Dkt. Kijaji kupitia bodi hiyo amewaelekeza Makamishna wa Uhifadhi nchini kusimamia ipasavyo maeneo ya uhifadhi na kuzuia shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na uendelezaji wa makazi karibu au ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa ili kuzuia migongano na athari zinazosababishwa na wanyapori wakali na waharibifu.

Kuhusu ujangili Dkt. Kijaji ametaka kuwepo na mipango na mikakati madhubuti ya utoaji wa elimu ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa Wananchi ipasavyo ili wajione kuwa ni sehemu ya uhifadhi jambo litakalosaidia kuendeleza uhifadhi na kupunguza ujangili.

Ameongeza kuwa ni dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ifikapo mwaka 2030 anaacha tabasamu kwa wananchi na kuwawezesha kunufaika na rasilimali za taifa.

“Katika eneo la migongano baina ya binadamu na wanyamapori ni lazima tuweke mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu ili kukabiliana na changamoto hizi kwa ufanisi,” amesema Dkt. Kijaji.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Dkt. Kijaji amesema TAWA imefanya vizuri, lakini amesisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato kupitia usimamizi bora wa rasilimali za wanyamapori.

Aidha, ameitaka Bodi hiyo kuweka malengo yenye uhalisia na yanayopimika katika mapambano dhidi ya ujangili, sambamba na kuandaa mikakati madhubuti ya kuyatekeleza. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda maeneo ya hifadhi na kufanya tathmini za kina kuhusu changamoto mbalimbali, ikiwemo uvamizi wa maeneo ya uhifadhi, ili kuweka hatua stahiki za kukabiliana nazo.

Kwa upande wa mahusiano na wananchi, Dkt. Kijaji amewataka askari wa uhifadhi kujenga ushirikiano mzuri na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kwa kuonyesha urafiki na kutoa huduma kwa weledi, jambo litakalorahisisha utatuzi wa changamoto za uhifadhi.

Aidha, amewapongeza kwa mafanikio yaliyopatikana katika maeneo ya uwekezaji na kuwataka kuendelea kusimamia ipasavyo maeneo ya uwekezaji pamoja na WMAs zote.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amesema Bodi ya TAWA imeendelea kufanya kazi nzuri katika kutekeleza majukumu yake ya msingi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Mej. Jenerali Semfuko, amesema bodi hiyo itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kuhakikisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori unaimarishwa na malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa ufanisi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!