Sakata la kisheria linalomkabili mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage, limeendelea kuibua mijadala mipana nchini baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha, kuibuka na kutoa tahadhari kuhusu usalama wa uhuru wa mawazo na fikra huru katika taasisi za elimu ya juu.
Kauli ya Dkt. Rioba inakuja kutokana na hatua ya mhadhiri huyo kutuhumiwa kufanya kosa la ugaidi, hatua inayowafanya wadau wa haki za binadamu na wanazuoni kufuatilia kwa karibu mwenendo wa shauri hilo.
Katika andiko lake alilolitoa kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Dkt. Rioba amefafanua kuwa ingawa hana uhakika wa kina kuhusu maudhui ya tuhuma zinazomkabili mhadhiri huyo wa UDOM, taifa halipaswi kuruhusu hali hiyo ya kujenga hofu inayoweza kuminya fikra huru.
“Sina uhakika na aina ya maudhui ya mhadhiri wa UDOM anayetuhumiwa kwa ‘ugaidi’, lakini ninashawishika kusema, kama Taifa, tusijiruhusu kufika huko! Tutakuwa Taifa la watu wajinga sana tukifika pahala tukadhani uhuru wa kufikiri, kuhoji na kukosoa unamilikiwa na watu fulani!” ameandika Dkt. Rioba.
Mwanahabari huyo mkongwe na msomi amesisitiza kuwa jukumu kuu la elimu ya chuo kikuu ni kuwajengea uwezo wa kutafakari kwa kina wale wanaosoma. Ameongeza kuwa, mchakato huo wa kitaaluma lazima ufanyike kwa misingi ya kisomi na siyo vinginevyo.
Hata hivyo, Dkt. Rioba amenyoosha kidole pia kwa upande wa wanazuoni akieleza kuwa endapo uchambuzi au utoaji wa taarifa unafanyika kwa mfumo wa harakati zisizo na tafakuri sahihi, nayo inakuwa ni changamoto nyingine.
Akihitimisha hoja yake, Dkt. Rioba ameeleza msimamo wake wa kutosimamia au kuunga mkono hatua yoyote inayolenga kudidimiza uhuru wa kutoa maoni, akitaja kuwa uhuru huo ndio nguzo kuu ya mfumo wa kidemokrasia.
“Siamini kabisa katika jitihada zozote za kufifisha uhuru wa mawazo au maoni katika demokrasia na haswa katika vyuo vikuu,” ameandika.
Ikumbukwe kuwa Kaijage alikamatwa 8 Julai 2026 kwa tuhuma za uchochezi wa maandamano ya umma ya tarehe 7 Julai, kosa ambalo awali alinyimwa dhamana. Kutokana na hatua hiyo, Chama cha Wanataaluma cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) kiliwasilisha maombi mahakamani kuomba apewe dhamana, ambapo shauri hilo lilisikilizwa Jumanne, tarehe 21 Julai 2026. Baada ya usikilizwaji huo, Mahakama ilitoa miongozo iliyomwezesha Mhadhiri Kaijage kukidhi vigezo vya kupata dhamana.
Hata hivyo, wakati mawakili wa utetezi na viongozi wa UDOMASA wakiwa katika mchakato wa kutekeleza amri hiyo ya mahakama ili kumtoa nje kwa dhamana, hati yake ya mashtaka ilibadilishwa na kusomewa mashtaka mapya ya ugaidi ambayo hayana dhamana.