Latest Posts

ASKOFU BAGONZA AHOJI HERUFI “M” NDANI YA CCM, ASEMA CHAMA HICHO NDICO BABA WA HARAKATI

Mjadala kuhusu dhana ya uanaharakati na nafasi yake katika historia na ustawi wa taifa la Tanzania unazidi kutawala katika majukwaa mbalimbali ikiwamo yale ya mitandao ya kijamii, kutokana na kauli iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 9, 2026, visiwani Zanzibar, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa maridhiano ya kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo.

Katika hotuba hiyo, Dkt. Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Taifa  aliwaonya ‘watu wanaojivika mwavuli wa uanaharakati’ ili kupata umaarufu wa kimataifa, huku nyuma ya pazia wakisukumwa na maslahi binafsi na vitendo vyenye viashiria vya kigaidi vilivyojificha kwenye sura ya uzalendo. Rais alisisitiza kuwa serikali haitafanya mzaha na vitendo vyote vya kigaidi na akawataka Watanzania kushikamana kwa ajili ya maendeleo badala ya kufuata makundi yenye ajenda zilizofichika.

Katika kile ambacho kimeelezwa kuwa mwendelezo wa utoaji maoni juu ya kauli ya Dkt. Samia, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza kupitia ukurasa wa Facebook amekumbusha kuwa herufi “M” katika jina la CCM inasimama badala ya “Mapinduzi,” ambayo amesema kimsingi ndiyo kilele cha juu kabisa cha uanaharakati. Askofu Bagonza amefafanua kuwa chama tawala ndicho chimbuko kuu la harakati nchini, akitolea mfano hatua ya TANU kujitenga na starehe za chama cha kijamii cha TAA ili kupigania uhuru, pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 chini ya ASP yaliyoleta ukombozi wa kweli.

“Mwaka 1967, TANU ilizindua Azimio la Arusha baada ya kukiri kuwa “tumenyonywa vya kutosha na sasa tunataka mapinduzi ili tusinyonywe tena”. Azimio la Arusha lilipindua meza na kuwafanya watwana kuwa mabwana. Hizo ni harakati. Mwaka 1977, TANU na ASP viliungana na kuunda CCM. Chama chenye historia ya kumwaga damu (ASP) kikaungana na chama chenye historia ya kudai haki kwa fikra kali na pevu (TANU). “Mapinduzi” ilikuwa ni alama wazi iliyowakilishwa na jembe na nyundo katika utambulisho wake. Ni harakati bado”, ameandika Dkt. Bagonza.

Kiongozi huyo wa kiroho amesisitiza kuwa chini ya mifumo ya asili ya TANU na CCM, ulinzi wa taifa ulikuwa mikononi mwa wananchi wenyewe, na vyombo vya dola vilitazamwa kama watumishi wa umma na sio zana za kukandamiza wanyonge kama inavyotazamwa sasa na baadhi ya Watanzania.

“Kimsingi, CCM ndiye baba wa harakati, nguzo ya haki na mpinga dhuluma popote duniani. Isimame ihesabiwe na isiwaache wapinzani kujitwalia utukufu kwa tunu za CCM. Yaliyotupata yote ni kwasababu tumeacha na kubeza harakati. Taifa lisilo na harakati ni sawa na pango la wanyang’anyi. Wanyonge ni kitoweo cha wenye nguvu. Taifa linajengwa na wenye moyo na kuliwa na wenye meno. Shangingi la Kijaluo linaimba, “Ukitoka na mume wangu, napita na baba yako ili uniite mama yako na mimi nikuite mke mwenza. Mama mkwe akikuzingua, mzingue binti yake mtaheshimiana””, amehitimisha Dkt. Bagonza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!