Latest Posts

WATU 17 WATUHUMIWA KWA UGAIDI SHINYANGA, 7 NI VIONGOZI WA CHADEMA AKIWAMO MNYAWAMI

Jumla ya watu 17 wakiwamo viongozi 7 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti pamoja na wanachama wengine wa chama hicho, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga wakikabiliwa na mashitaka yanayohusu ugaidi, siku ya Ijumaa, Julai 24, 2026.

Miongoni mwa viongozi waliopandishwa kizimbani ni pamoja na Jackson Mnyawami (Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti), Hamis Ngunila (Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini), na Salum Mwinyi (Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA – BAZECHA Wilaya ya Kahama), huku wengine wanne wakiwa ni viongozi wa chama hicho ngazi ya kata mkoani humo.

Washitakiwa hao wamegawanywa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza linamjumuisha Jackson Mnyawami, Daniel Emmanuel Athumani, na Jackson Venant Kabyeseleza. Hawa wanatuhumiwa kupanga kutenda kosa la ugaidi kwa kuuchochea umma kufanya maandamano mnamo Julai 7, 2026.

Kundi la pili lina watu 14 wanaotuhumiwa kwa kosa la kula njama za kutenda ugaidi. Wanaoshitakiwa katika kundi hili ni Godwine Laurent, Johnson Paul Michael, Joseph Isack Ongoro, Edwin Otieno Ongito, Jabari Abdul Sharifu, Sengiyumba Sadiki, Boniphace Kwini Kasuluba, Hussein Marijani Hamidu, Mohamed Shaban Nkimani, Mwinyi Salum Kulyengana, Omary Ally Ng’haniga, Maulid Ramadhan, Hamisi Ngunila, pamoja na Mhebi Charles Yoyo.

Kiini cha mashitaka hayo kinatokana na madai ya upande wa Jamhuri kuwa washitakiwa walihamasisha na kupanga maandamano yasiyo halali mnamo tarehe 7 Julai, 2026, kitendo kinachodaiwa kilihatarisha usalama wa nchi.

Akizungumza na Jambo TV, Wakili Alex Massaba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, ameelezea mazingira ya kukamatwa kwa baadhi ya washitakiwa kuwa ni ya kusikitisha. Alitolea mfano wa Mzee Salum Mwinyi aliyekamatwa akiwa njiani kwenda kumdhamini mfanyabiashara mwenzake, na Mnyawami ambaye alikamatwa alipokwenda kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) Shinyanga kwa jambo lingine. Aidha, Wakili Masaba amedai kuwa mashitaka hayo yana lengo la kuwakomoa viongozi wa kisiasa wa chama hicho badala ya kutafuta haki.

Kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kusikiliza kesi za aina hiyo, washitakiwa wote wamepelekwa katika Gereza la Shinyanga hadi tarehe 4 Agosti, 2026, kesi itakapotajwa tena.

Wakati huo huo, mtuhumiwa mwingine ambaye ni Fredy Masanja, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Wilaya ya Shinyanga, naye alirejeshwa mahabusu bila kusomewa mashitaka baada ya kubainika kuwa Hati yake ya Mashitaka ilikuwa na makosa ya kiufundi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!