Latest Posts

AIRTEL AFRICA YAINGIZA DOLA BILIONI 1.85 KATIKA ROBO YA KWANZA, MAPATO YAKUA KWA ASILIMIA 31

Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Africa imeanza mwaka wa fedha 2026/27 kwa mafanikio baada ya kurekodi mapato ya dola bilioni 1.853 za Marekani katika robo ya kwanza iliyoishia Juni 30, 2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na dola bilioni 1.415 zilizopatikana katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema ukuaji huo umechangiwa na ongezeko la matumizi ya huduma za intaneti, simu janja na Airtel Money katika nchi 14 ambazo kampuni hiyo inahudumu, ikiwemo Tanzania.

Faida baada ya kodi iliongezeka kwa asilimia 27 na kufikia dola milioni 198, huku mapato kwa viwango vya fedha visivyobadilika (constant currency) yakikua kwa asilimia 21.1. Ukuaji ulionekana katika huduma za sauti, intaneti na huduma za kifedha kwa njia ya simu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, soko la Nigeria liliongoza kwa ukuaji wa asilimia 29.8, likifuatiwa na ukanda wa Afrika ya Kati na Magharibi unaozungumza Kifaransa kwa asilimia 18, wakati Afrika Mashariki ilirekodi ukuaji wa asilimia 17.8.

Idadi ya wateja wa Airtel Africa iliongezeka kwa asilimia 11.6 na kufikia milioni 189, huku asilimia 51 ya wateja wote wakitumia simu janja. Wateja wa intaneti waliongezeka kwa asilimia 15.5 hadi milioni 87.3, wakati wastani wa matumizi ya data kwa kila mteja uliongezeka kutoka GB 7.8 hadi GB 10.6 kwa mwezi, na kusababisha matumizi ya data kuongezeka kwa asilimia 56.3 ndani ya mwaka mmoja.

Huduma ya Airtel Money nayo iliendelea kufanya vizuri, ambapo idadi ya wateja iliongezeka kwa asilimia 23.3 na kufikia milioni 56.5. Thamani ya miamala iliyofanyika kupitia huduma hiyo ilifikia zaidi ya dola bilioni 245 kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko la asilimia 51.5, huku mapato ya Airtel Money yakiongezeka kwa asilimia 38.9 na kufikia dola milioni 404.

Katika robo hiyo, Airtel Africa iliwekeza dola milioni 389 kupanua miundombinu yake, ikijenga zaidi ya minara na vituo vipya vya mawasiliano 920 pamoja na kuongeza mtandao wa nyaya za mawasiliano (fibre) hadi kufikia kilomita 82,100.

Aidha, mapato kabla ya riba, kodi, kushuka kwa thamani na malipo ya madeni (EBITDA) yaliongezeka kwa asilimia 36.6 hadi dola milioni 928, huku kiwango cha faida cha EBITDA kikifikia asilimia 50.1. Fedha taslimu zitokanazo na shughuli za uendeshaji nazo ziliongezeka kwa asilimia 38.3 hadi dola milioni 786.

“Tumeanza mwaka huu kwa matokeo mazuri. Kuongezeka kwa matumizi ya simu janja, ushiriki mkubwa wa wateja katika huduma za kidijitali na uwekezaji unaoendelea katika miundombinu vinaendelea kuchochea ukuaji wetu,” alisema Taldar.

Pia alibainisha kuwa Airtel Africa inaendelea na maandalizi ya kuorodhesha biashara ya Airtel Money katika Soko la Hisa la London (LSE) baada ya kupata idhini kutoka kwa mamlaka husika, hatua inayolenga kuongeza thamani ya biashara hiyo na kuvutia wawekezaji zaidi wa kimataifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!