Latest Posts

SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU

Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi za watetezi wa haki za binadamu nchini huku ikitoa wito kwa wadau wa maendeleo wa kimataifa kuendelea kuziunga mkono taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 15 wa Wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) uliofanyika leo Ijumaa Julai 24, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema mchango wa washirika wa maendeleo umekuwa na manufaa makubwa kwa taasisi hizo na kwa maendeleo ya haki za binadamu.

Balozi Nchimbi amewashukuru wadau hao wa kimataifa kwa ushirikiano wao na kumwomba Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania kufikisha salamu za shukrani kwa washirika wengine wa maendeleo.

Amesema kupitia rasilimali fedha ambazo wadau hao wamekuwa wakizitoa, taasisi na asasi mbalimbali zimefanikiwa kuongeza ajira kwa Watanzania pamoja na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za kutetea haki za binadamu.

Aidha, Mhe. Nchimbi amewataka washirika wa maendeleo kutoona tabu kuendelea kujadili namna ya kuimarisha msaada wao kwa taasisi za ndani, akieleza kuwa kupungua kwa michango kutaathiri moja kwa moja uwezo wa watetezi wa haki za binadamu kutekeleza majukumu yao.

“Wanapopunguza michango yao wanapunguza nafasi muhimu kwa watetezi wa haki za binadamu, si kwa Tanzania tu bali Afrika na dunia kwa ujumla,” amesema.

Aidha ameongeza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau hao, huku ikiwahimiza kuendelea kutoa usaidizi kadri itakavyowezekana ili kuhakikisha taasisi hizo zinaendelea kuwa na mchango chanya kwa jamii.

Mkutano huo wa 15 wa Wanachama wa THRDC umewakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala yanayohusu ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!