Latest Posts

USHAHIDI WA ACP MAHAMBA: KAULI ZA LISSU ZILILENGA KUITISHA SERIKALI

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu inaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ambapo shahidi wa Jamhuri Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP), Amin Mahamba ametoa ushahidi wake mbele ya mahakama hiyo.

ACP Mahamba amesema anafanya kazi Makao Makuu Ndogo ya Jeshi la Polisi Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini( DCI), ofisi ambayo ipo Dar es Salaam katika Kitengo X kinashughulikia makosa ya mtandao na makosa yanayotishia usalama wa nchi na migogoro huku akiwa na uzoefu wa miaka 26 kwani ameajiriwa mwaka 2000.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga ameieleza mahakama namna alivyoweza kuongoza timu ya upelelezi juu ya jalada la uhaini la Tundu Lissu.

Shahidi ACP Mahamba mbele ya jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru ameeleza kuwa kauli alizotoa Lissu katika video iliyochapishwa Youtube na Jambo TV ni kauli ambazo zilikuwa zinaitisha serikali.

 

UZOEFU WA SHAHIDI KATIKA KAZI YAKE

Anaeleza kuwa amepata mafunzo ya awali, Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi, kuanzia mwaka Agosti 2000 hadi 2001 katika kozi hiyo anakumbuka alijifunza masomo mbalimbali, ikiwemo uchunguzi wa Kijinai, masomo ya Sheria mfano Sheria ya Ushahidi, Sheria ya Ulinzi wa mashahidi, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sheria ya Kanuni ya Adhabu na mbinu za kijeshi.

Akajifunza mbinu za kijeshi mafunzo ya kivita anaeleza kufanya kazi ya upelelezi Tanga kwa miaka mitano ambapo alikuwa chini ya ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi Chumbageni. Mwaka 2006 kwa kipindi cha miezi mitatu alihudhuria mafunzo maalum katika Chuo cha Polisi CCP Moshi ambayo yalijikita katika mbinu mbalimbali za upelelezi baadae akahitimu na kupewa cheti cha ufaulu.

Kutokana na kuwa na ufaulu mzuri akateuliwa kuwa Mwalimu wa Upelelezi CCP(Chuo cha Taaluma ya Polisi) akiwa na majukumu ya kufundisha masomo mbalimbali ikiwemo somo la upelelezi pamoja na masomo mengine kadiri alivyopangiwa na viongozi wake akifanya kwa miaka mitatu 2006-2009.

Aliendelea kupata uzoefu wa upelelezi ambapo mwaka 2014 aliteuliwa na IGP kuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya Kyela mkoani Mbeya akiwa msimamizi mkuu wa maafisa wote wapelelezi akihudumu katika nafasi hiyo mpaka mwaka 2016.

Mwaka 2017 ACP Mahamba alihamishiwa Mkoa wa Ruvuma na kuwa Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoa huo(RCO) akiwa na majukumu ya kusimamia mkoa kama mkuu wa wapelelezi wote. Akikaa mkoa huo kwa miaka mitano (2017-2022)

Mwaka 2023 akahamishiwa jijini Dar es Salaam na kuwa msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya jinai wa kanda hiyo(Deputy ZCO) akikaa kwa miezi kumi januari mpaka oktoba na baadae kuhamishiwa mkoa wa kipolisi Kinondoni na kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuanzia Oktoba 2023 na mwaka 2024 alihamishiwa ofisi anayohudumu sasa iliyopo kitengo X Makao Makuu Ndogo ya Polisi Dar es Salaam.

ACP MAHAMBA ALIVYOPELELEZA VIDEO ZA LISSU

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Katuga ACP Mahakamba anadai April 8, 2025 majira ya mchana akiwa ofisini kwao Makao Makuu Ndogo ya Polisi iliyopo katikati ya jiji(Posta) alipewa maelekezo na Afande Ramadhani Ng’azi kwamba afike Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalum Dar es Salaam kwenda kusimamia na kuratibu upelelezi wa jalada la uhaini ambalo lilikuwa tayari limefunguliwa Ofisi ya ZCO Kanda Maalum ambalo lilikuwa linamhusu Tundu Atiphas Lissu.

Anaeleza kuwa kitengo chao kinajihusisha masuala ya uhaini. Na alitakiwa kwenda kuonana na Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda ACP George Bagyemu na alipofika katika ofisi zilizopo karibu na kituo cha SGR.

Alipofika alikutana ACP George akamuingiza ofisini kwake na kumtambulisha kwa timu yake ya upelelezi na kumpa mrejesho walipofikia katika upelelezi wa jalada la uhaini kisha aliipangia majukumu timu wapo wapelelezi waliopewa kazi za operesheni ikiwemo kukamata, kupekua na wengine aliwapa jukumu la kukusanya taarifa huku timu nyingine ikikusanya ushahidi na kuuchakata.

Baada ya kumaliza kugawa majukumu wote walianza kuitazama video ambayo ilikuwa kwenye mtandao wa  Youtube akaunti ya Jambo TV ikimuonyesha mshtakiwa Tundu Lissu akihutubia.

Anaeleza katika Ofisi hiyo kuna kompyuta maalum ya Polisi inayotumiwa na Asistance Inspekta Michael yenye intaneti ya polisi wakiitazama video hiyo ya Lissu mwanzo mpaka mwisho kwa takribani masaa mawili huku Lissu akiwa amevalia kombati maarufu ya CHADEMA nyuma yake kukiwa na bendera ya taifa na bendera ya CHADEMA alikuwa kavaa miwani huku akitumia lugha ya taifa.

Baada ya kumaliza kutazama video hiyo ACP Mahamba anaeleza kuwa walibaini yale maneno aliyokuwa akitamka mshtakiwa yalikuwa ni kosa ambalo anashtakiwa nalo la uhaini.

Anadai kuwa Lissu alitamka akisema “wanasema kitu kimoja sahihi hapa msimamo huu unaashiria uasi ni kweli kwa sababu tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi hiyo ndiyo namna ya kupata mabadiliko kwa sababu tunaenda kukinukisha sana sana. Huu uchaguzi tutauvuruga kwa sababu tunaenda kukinukisha vibaya sana“

Anaendelea kueleza kuwa yeye pamoja na timu yake waliona kwamba mshtakiwa Lissu alikuwa na nia ya kuitisha serikali ili itende kile anachotaka kitendo cha kuitisha serikali kwa kuzuia uchaguzi kwa kuhamasisha uasi ndio uhaini wenyewe.

Anasema kosa la uhaini limeiainisiwa kifungu cha 39(a)(b) kwa mujibu wa uchunguzi wao  walichunguza wakabaini kwamba Lissu ni raia wa Tanzania na kwakua ni Raia wa Tanzania ana wajibu wa kutii Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa ndani au nje ya nchi

Anafafanua kuwa maneno ‘tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi na tutavuruga uchaguzi” hayo maneno ni ya kutisha serikali kwa sababu serikali ina wajibu wa kulinda amani ndani ya nchi na hayo maneno yana viashiria vya kuvunja amani hivyo kutamka hayo maneno ni kuitisha serikali.

Anaeleza kuwa waliona mshtakiwa alitenda kosa la uhaini alidhihirisha nia yake ya kuitisha serikali kwa kuchapisha taarifa kwa umma kupitia mtandao wa kijamii Youtube wa Jambo TV.

Anaeleza kuwa uchaguzi uliokuwa unazungumziwa ni uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa 2025 ambao upo kwa mujibu wa katiba na sheria.

Akiulizwa na Wakili Katuga pale ambapo katiba inapokuwa inavunjwa mlinzi wake ni serikali.

Kuvuruga uchaguzi anayeathirika mmoja ni serikali ambaye anahusika kusimamia na ndiye mwenye jukumu la kusimamia

Anaeleza kuwa katika upelelezi wao haya maneno kukinukisha yalilenga matendo ambayo yangeweza kuzuia uchaguzi kwa kutumia mbinu mbalimbali kuzuia wapiga kura wasipige kura.

Anasema maneno yaliyotamkwa na Mshtakiwa ‘tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi tutavuruga uchaguzi kwa sababu tunaenda kukinukisha vibaya san’ haya maneno ni maneno yenye vitisho dhidi ya serikali. Hivyo kutamka maneno hayo kuzuia uchaguzi ni kinyume na katiba na sheria za nchi hii.

Anaeleza anachokumbuka baada ya upelelezi na kukusanya vielelezo, vielelezo vyote ambavyo ni video iliyopatikana kwenye Youtube ya Jambo TV na Memory card vilifikishwa maabara ya uchunguzi kuchunguza picha lengo ikiwa ni kufanya uliganifu kama picha mjongeo iliyopatikana kwenye Youtube inafanana na picha ambayo ilipatikana kwenye Memory.

Anadai shahidi uchunguzi ulifanyika na kupata taarifa ya uchunguzi walibaini kuwa ile picha mjongeo iliyopatikana kwenye mtandao wa Youtube na ile iliyopatikana kwenye memory card ndiyo hiyo moja.

Anakumbuka siku hiyo ya April 8, 2025 alimuelekeza Afande Michael aende maabara ya uchunguzi akachukue vielelezo ambavyo vimechunguzwa pamoja na taarifa ya uchunguzi ambapo alifanya hivyo kutoka pale maabara ya uchunguzi na kisha kurudi ofisini na kukabidhi kwa mtunzaji wa vielelezo

Akapiga simu kwa Wakuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Nchini kuwa lengo hasa ni kutaka kujua ni kwa kiasi gani ile kauli ya Lissu jamii imepokeaje. Baadhi ya maRCO wakamwambia wana taarifa hizo na baadhi ya watu wamewakamata baada ya kuwakuta kuchochea kushawishi wengine kula njama ya kufanya maandamano akitaja mikoa kama Arusha, Kilimanjaro, Mbeya Ruvuma na Dar es Salaam.

Anaeleza kuwa aliitisha majalada kutoka mikoa hiyo la uchunguzi kutoka kwa mikoa houo na baada ya kuitisha hayo majalada timu iliyapokea na kuanza kuyasoma na kuyapitia kwa pamoja walibaini wengi waliokuwa mle waliokuwa wamehamasika na kauli ya mshtakiwa na wengi wao walikuwa wafuasi na wanachama wa CHADEMA.

Alielekeza kuwa watu hao watafutwe wapatikane na waandike maelezo kama mashahidi wa athari zilizotokana na kauli za Lissu katika kesi ya uhaini walipatikana na kutekeleza maelekezo.

April 9, 2025 ndiyo tarehe ambayo mshtakiwa Tundu Lissu alikamatwa akiwa ziarani na kusafirishwa kutoka Mbinga na kuletwa Dar es Salaam kituo cha kati(Central Police) na kupelekwa moja kwa moja ofisi ya Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Pwani ikiwa ni tarehe 10 april 2025.

Baada ya kufikishwa Lissu alipelekwa mbele ya Deputy ZCO George Bagyemu alimsomea tuhuma zake lakini mshtakiwa.

Baada ya kupata maelezo ya Lissu, jalada lilifikishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya maamuzi mengine ya kisheria na ilipofika majira ya mchana ofisi hiyo iliandaa mashtaka dhidi ya mshtakiwa na kumfikisha mahakamani siku hiyo hiyo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la uhaini

 

VITISHO DHIDI YA MASHAHIDI

Anaeleza anakumbuka baada ya Lissu kusomewa mashtaka yake jalada la upelelezi lilirudishwa kwao kwa ajili ya kukamilisha upelelezi ambapo walipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya mashahidi kupitia Wakuu wa Upelelezi wa Mkoa kwamba wanaweza kupata madhara endapo watakuja kutoa ushahid mbele ya mshtakiwa.

Anaeleza kuwa matishio hayo wahusika waliyaona kupitia mitandao ya kijamii na wengi wao walikuwa wafuasi wa CHADEMA wakitamka maneno kwamba ‘watawadhuru mashahidi endapo wakienda kutoa ushahidi’ wakisema watawasalimia endapo wakienda kutoa ushahidi wengine wakasema watawaombea mabaya.

Anaeleza kuwa walifanya upelelezi wakajiridhisha kama hayo malalamiko yana ukweli wakajaribu kupitia baadhi ya mitandao kwenye comments kulikuwa na vitisho kupitia Instagram, Facebook, tiktok.

Baada ya kuthibitisha yeye kama mpelelezi mkuu aliwasiliana na ofisi ya taifa ya mashtaka kuhusu matishio lengo ikiwa ni kama kuna uwezekano wa kuombea ulinzi waombe na ofisi hiyo iliweka kiapo maalum maombi ya kinga kwa mashahidi ambao wanapitia hali ya matishio

Baada ya hapo shahidi ACP Mahamba akawa amemaliza kutoa ushahidi wake na kuruhusu maswali ya dodoso kutoka kwa mshtakiwa Tundu Lissu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!