Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania kulinda amani, usalama, na utulivu kama nyenzo kuu ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.
Akizungumza wakati akihitimisha Tamasha la Kizimkazi Festival leo Ijumaa, Agosti 14, 2026 visiwani Zanzibar, Dkt. Samia amesisitiza kuwa mafanikio yanayoonekana katika sekta za uwekezaji na huduma za jamii yanategemea uwepo wa hali ya utulivu. Amewataka wananchi kutochukulia tunu hizo kama jambo la kawaida, bali wazitunze kwa nguvu zote.
Mkuu huyo wa nchi amebainisha kuwa mipango mikubwa ya serikali katika kuvutia utalii, biashara, na kutengeneza ajira haiwezi kufanikiwa ikiwa nchi itaingia katika machafuko. Ameeleza kuwa amani ni kila kitu katika maisha ya binadamu na ndiyo roho ya maendeleo yoyote.

“Uwekezaji, maendeleo tunayoyaona hapa; uwekezaji, utalii, biashara, ajira na huduma za jamii hayawezi kustawi katika mazingira ya vurugu na uvunjifu wa amani. Niwaombe Watanzania wenzangu hususan vijana msikubali kuharibu amani ya nchi yenu. Amani ndio kila kitu katika maisha yetu,” amesisitiza Dkt. Samia.
Katika hatua nyingine, Rais amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kukataa ushawishi wa watu au vikundi ambavyo havina nia njema na mustakabali wa taifa. Amesema kuwa ulinzi wa Tanzania na Muungano wake ni jukumu la kila mmoja ili kuhakikisha vizazi vijavyo vinarithi nchi yenye utulivu.
“Kwa hiyo niwaombe sana tukatae kwa nguvu zote wasiolitakia mema taifa letu na tulinde Tanzania yetu na muungano wetu kwa mustakabali wa kizazi chetu na kizazi kijacho,” ametoa rai Rais Samia huku akishangiliwa na umati wa watu.
