Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amepuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa uhusiano mbaya kati ya jeshi la polisi na wananchi, akieleza kuwa jeshi hilo ni sehemu ya jamii na dhana ya watu kuliogopa imepandikizwa kwa malengo ya kisiasa
Akizungumza katika mahojiano maalum na DW Kiswahili, Katambi amesisitiza kuwa askari polisi na wanajeshi nchini Tanzania si watu kutoka “dunia ya tatu,” bali ni ndugu, jamaa, na majirani wa Watanzania wenyewe. Amebainisha kuwa askari hawa ndio watu ambao wananchi wanasali nao makanisani, misikitini, na wamesoma nao mashuleni.
“Mazuri sana, mimi nikitaka kuwauliza kwa mfano, lini yaliharibika? Yaani lini yaliharibika mahusiano kati ya wananchi na jeshi kwa sababu wanajeshi wote wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama hapa Tanzania nzima aidha ni kaka zetu, ni watoto wa shangazi, wa mjomba, kama sio wa mjomba, ni wa jirani zako. Kwani polisi hao wanatoka dunia ya tatu? Wanajeshi wanatoka dunia ya tatu. Vyote, vyombo vya ulinzi na usalama ni wanatokana na sisi, si wanatokana na jamii, ndio hao tulikuwa tunasali nao kanisani au tunaenda nao madrasa au sio? Au Sunday school au tumesoma nao shuleni. Ni sehemu ya jamii, na kama ni sehemu ya jamii tafsiri yake ni kwamba ni ndugu zetu”, ameeleza.
Akijibu hoja kuhusu hofu iliyopo miongoni mwa wananchi dhidi ya vyombo vya ulinzi, Waziri Katambi ameweka wazi kuwa hakuna sababu ya raia mwema kuwa na hofu.
“Mhalifu pekee ndio ataogopa… ni ile tu dhana potofu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu sana kutaka tu kuonesha kwamba hawa watu ni hivi wakati labda nini hapana,” amesema Katambi akirejea utaratibu wa wananchi kuomba lifti kwenye magari ya askari kama ishara ya ukaribu
Katambi amedai kuwa chuki inayozungumzwa dhidi ya polisi ni matokeo ya “propaganda” na “mapandikizi ya kisiasa” yenye lengo la kuaminisha umma kuwa nchi ina matatizo ili baadhi ya taasisi au watu waweze kunufaika.
“Kwa sehemu kubwa sana ni mapandikizi ya kisiasa… ni wakati mwingine kutaka kuaminisha watu kwamba always we have a problem. Hakuna taasisi yoyote ambayo inaweza ika-operate kama hakuna matatizo,” amesisitiza Waziri huyo
Waziri amewakumbusha wananchi kuwa polisi ndiye “mbabe wa mwisho” katika kulinda mali na haki za raia pindi wanapoonewa au kudhulumiwa. Amesema kuwa iwapo mwananchi anaibiwa hata simu yake au kudhulumiwa shamba, kimbilio lake la kwanza ni polisi, hivyo hakuna mantiki ya kuwepo kwa chuki.