Mtu mmoja anadaiwa kufariki dunia baada ya gari aina ya Toyota Alphard, lenye namba za usajili T. 837 EMS, kugongana uso kwa uso na basi la ZUGGPI TZE, lenye namba 636 AQN, katika eneo la King’ori, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Agosti 8, 2026,wakati dereva wa basi hilo akidaiwa kuyapita magari mengine bila tahadhari na kisha kugonga gari hilo dogo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Tanga kuelekea Arusha, huku gari dogo aina ya Toyota Alphard likielekea Arusha mjini, kabla ya magari hayo kugongana uso kwa uso katika eneo hilo.

Baada ya ajali hiyo kutokea basi hilo liliteketea kwa moto kabla ya vikosi vya jeshi la zimamoto na uokoaji kufika na kuuzima moto huo
Aidha, aliyefariki anadaiwa kuwa raia wa kigeni, aliyekuwa akisafiri na gari dogo lililohusika kwenye ajali hiyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo huku watu waliojeruhiwa wanaendelea kupatiwa matibabu.