Wakili wa Kujitegemea, Peter Madeleka, ametangaza nia ya kufungua kesi mahakamani kupinga tangazo la Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania linalowapiga marufuku mawakili kuzungumza na vyombo vya habari ndani ya viunga vya mahakama. Madeleka amedai kuwa zuio hilo ni ukiukwaji mkubwa wa Ibara ya 18(b) ya Katiba inayotoa haki ya kutafuta, kupata, na kutoa habari bila kujali mipaka
Hatua hii inakuja kufuatia tangazo lililotolewa na Msajili wa Mahakama Kuu, C.M. Tengwa, mnamo Agosti 12, 2026, ambalo liliwakumbusha mawakili kuzingatia Kanuni ya 137 ya Maadili ya Mawakili na Ibara ya 30(1)(2)(d) ya Katiba. Tangazo hilo lilisisitiza mawakili kutohojiwa na vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa mashauri yanayoendelea kwa namna inayoweza kuathiri utoaji haki
Akizungumza na wanahabari leo Agosti 14, 2026, Madeleka amekosoa vikali tafsiri ya kisheria iliyotumiwa na Msajili. Amesema kuwa kutumia Ibara ya 30(1) kuwazuia mawakili ni kutokuielewa Katiba, kwani ibara hiyo inazuia tu haki ya mtu mmoja isiingilie uhuru wa mwingine, na si kupiga marufuku mawasiliano
“Kutumia ibara ya 30 ibara ndogo ya kwanza ya katiba ya jamhuri ya muungano wa tanzania kuwapiga marufuku mawakili kutokuzungumza na vyombo vya habari… ni kuthibitisha kwamba aliyetoa hili tangazo haielewi,” amesema Madeleka kwa msisitizo
Aidha, amebainisha kuwa haki ya habari haipaswi kuishia “kwenye geti la mahakama,” na kuhoji ni nani aliyelalamika kuathiriwa na mahojiano ya mawakili
Wakili huyo amerejea Kifungu cha 192(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, akisema kesi zote za jinai lazima ziendeshwe kwenye mahakama ya wazi na si kwa siri.
“Uchawi pekee yake ndio unatakiwa kufanyika kwa siri wakati wengine wamelala usiku. Lakini sio kesi za uhujumu uchumi sio kesi za jinai,” amefafanua Madeleka
Madeleka amesisitiza kuwa yuko tayari kwa hatua zozote za kisheria, ikiwemo kupelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili ikiwa Msajili anaona anaathirika na kauli zake. Amesema kuwa Ibara ya 107B ya Katiba inataka mahakama izingatie katiba na sheria na si mitandao ya kijamii, hivyo mahojiano hayapaswi kuingilia uhuru wa mahakama.