Benki ya CRDB imeendelea kutoa zawadi kwa wateja wake kupitia kampeni ya “Bonge la Wakala”, inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za benki kwa njia ya simu pamoja na kufanya miamala kupitia mawakala wa benki hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa mshindi kwenye tawi la Geita, Meneja wa Mahusiano kutoka Ofisi ya Kanda ya Kidagaa, Peter, amesema kampeni hiyo imeendelea kutoa zawadi kwa wateja wanaofanya vizuri katika matumizi ya huduma za CRDB kupitia mawakala.
Katika kampeni hiyo, Omary Faustine Kazungu ameibuka mshindi na kukabidhiwa zawadi ya televisheni ya nchi 65, baada ya kufanya vizuri katika matumizi ya huduma za CRDB na kufanya miamala kupitia mawakala.

Peter amesema Omary ameshinda miongoni mwa wateja 10 waliofanya vizuri zaidi katika kipindi husika, huku akieleza kuwa kampeni hiyo itaendelea kuwafikia wateja mbalimbali.
Amesema CRDB itaendelea kutoa zawadi kupitia kampeni hiyo hadi kufikia jumla ya shilingi milioni 30, kwa mteja atakayefanya vizuri zaidi katika matumizi ya huduma hizo.
Kwa upande wake, Omary Faustine Kazungu, mshindi wa televisheni hiyo, amesema huduma za benki kwa njia ya simu zimekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.

Omary amesema amefurahishwa na ushindi huo, huku akiishukuru CRDB kwa kuendelea kuwazawadia wateja wanaotumia huduma zake.
CRDB imewataka wateja kuendelea kutumia huduma za benki kupitia simu na mawakala ili kupata fursa ya kushiriki katika kampeni hiyo na kujinyakulia zawadi mbalimbali.