Latest Posts

UOGA WA KUTEKWA: JAJI WARIOBA AFICHUA KWANINI WANANCHI HAWATOI MAONI YAO TENA

Jaji mstaafu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Joseph Sinde Warioba, ametoa onyo kali kuhusu hali ya usalama na uhuru wa kutoa maoni nchini, akibainisha kuwa sasa hivi Watanzania wanaishi katika hali ya uoga inayozuia ushiriki wao katika masuala muhimu ya kitaifa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na tovuti ya The Jenerali Ulimwengu Post, Jaji Warioba ameeleza kuwa mazingira ya hofu ya kutekwa na kupotea yanazuia wananchi kutoa maoni yao ya kweli juu ya mustakabali wa taifa

Jaji Warioba ameeleza kuwa tofauti na nyakati za nyuma, hivi sasa kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi wa kawaida kuhusu usalama wao binafsi. Amebainisha kuwa matukio ya watu kupotea yameacha kovu kubwa ambalo linaathiri hata michakato ya kiserikali inayohitaji maoni ya umma.

“Ukichukua wananchi kwa sasa hivi hawana uhuru kama ilivyokuwa, kwamba sasa hivi Watanzania wanaishi kwa uoga, sio kama ilivyokuwa wakati ule, wanaishi kwa uoga wanaishi kwa uoga, wanaogopa kutekwa, kupotea. Kwahiyo unakuta hata haya tunayoyafanya yote hupati maoni ya wananchi wanavyoona kwa sababu wanaogopa,” amesema Jaji Warioba

Kuhusu kuundwa kwa Tume ya Maridhiano, Jaji Warioba ametoa ushauri kuwa suala hilo ni mtambuko na halipaswi kushughulikiwa kama tume za kawaida za Rais ambazo hupewa hadidu za rejea na kuanza kazi bila ushirikishwaji mpana. Amesema ili tume hiyo iaminiwe, ni lazima Rais apate ushauri na mawazo kutoka kwa makundi mbalimbali kabla ya kuiteua.

Amesisitiza kuwa maridhiano ya kweli yanahitaji ushiriki wa watu wengi zaidi, wakiwemo wanasiasa, taasisi za dini, asasi za kiraia na kundi muhimu la vijana, ambao mara nyingi wamekuwa wakionesha hasira zao kupitia maandamano yanayokabiliwa na nguvu ya dola.

Jaji Warioba amesisitiza kwa kusema kuwa bila kutafuta njia ya kuwafanya vijana na raia wengine wajihisi kuwa sehemu ya mazungumzo, itakuwa vigumu kuiponya nchi kufuatia yaliyotokea Oktoba 2025. Amebainisha kuwa mchakato huo unapaswa kuwa kama Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kuleta mwafaka unaokubalika na pande zote.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!