Kutokana na kuongezeka kwa kasi ya uwekezaji katika shughuli za kuongeza thamani madini nchini na kujifungamanisha kwake na sekta nyingine za uchumi, Sekta ya Madini imeendelea kuweka msingi madhubuti wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa Dola Trilioni 1 kupitia viwanda.
Akiweka msisitizo huo Agosti 19, 2026 wakati wa ziara ya kikazi wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amebainisha kuwa ni jambo la kujivunia kuona Tanzania ikizalisha bidhaa za madini zinazouzwa kwenye mataifa makubwa duniani kama Marekani na nchi za Ulaya.

Akiwa wilayani humo kufuatilia shughuli za madini na kutoa maelekezo ya kisekta, Dkt. Kiruswa alitembelea viwanda vikubwa vya KEDA Tanzania Float Glass kinachozalisha vioo kwa ajili ya majengo na magari, pamoja na GoodWill Ceramic Co. Ltd kinachozalisha vigae na vifaa vya usafi wa majumbani.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa amesisitiza uzingatiaji wa bei elekezi zinazotolewa na Serikali kwa madini yanayotumika viwandani, huku akimuagiza Afisa Madini Mkazi Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuandaa semina kwa wamiliki wa viwanda na leseni za uchimbaji kuhusu uwajibikaji kwa jamii (CSR) na utunzaji wa mazingira.

Akiwasilisha maendeleo ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasri Ally, ameeleza kuwa wilaya hiyo ina viwanda 275 ambapo viwanda 39 vinatumia madini huku shughuli za madini zikichangia Shilingi bilioni 3.2 katika mwaka wa fedha 2025/26. Ameongeza kuwa wametenga ekari 15 kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu ili kurahisisha uhifadhi na usafirishaji wa bidhaa.
Kwa upande wa wawekezaji, Meneja Biashara wa KEDA Tanzania, Ruby Zhu, ameeleza kuwa asilimia 98 ya malighafi zao zinatoka Mkuranga huku wakizalisha tani 600 za vioo kwa siku. Naye Meneja Biashara wa GoodWill, Justin Xie, amebainisha kuwa asilimia 90 ya malighafi zao zinatoka nchini na kwamba kiwanda chake kimetoa ajira za moja kwa moja 3,000 na zisizo za moja kwa moja 12,000.
“Tumeweka mizizi nchini Tanzania, tunaweza kujitolea kubadilisha rasilimali za madini za ndani kuwa bidhaa za usafirishaji nje yenye thamani kubwa, na kuleta ajira zaidi na kodi na kushiriki na idara zote kuzungumzia vizuizi katika mnyororo wa usambazaji wa madini,” alisema Justin Xie.

Naye Afisa Madini wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Lameck Gabote, amehitimisha kwa kueleza kuwa Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya ujenzi na viwandani yanayohudumia kwa kiasi kikubwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.