Gazeti MwanaHALISI limesitishiwa leseni ya kuchapisha na kusambaza habari kwa kipindi cha miezi sita, baada ya Idara ya Huduma za Habari- MAELEZO, kubaini kuwa gazeti hilo limerudia makosa ya kitaaluma licha ya kupewa onyo hapo awali.
Kwa mujibu wa taarifa ya MAELEZO, hatua hiyo imechukuliwa baada ya gazeti hilo kuchapisha habari yenye kichwa “Nchimbi agoma kujiuzulu” katika toleo namba 571 la Agosti 6 hadi 12, 2026, huku likidaiwa kushindwa kuzingatia misingi ya usahihi na mizania ya habari kabla ya taarifa hiyo kuchapishwa na kusambazwa kwa umma.
Aidha, MAELEZO imebainisha kuwa gazeti hilo lilitumia picha ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, katika ukurasa wa pili, lakini maelezo yaliyowekwa chini ya picha hiyo yalimtaja kuwa ni Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. MAELEZO imesema kosa hilo linaonesha kuwepo kwa dosari katika uandishi na mnyororo mzima wa uhariri uliopaswa kuhakikisha usahihi wa taarifa kabla ya gazeti kuchapishwa.
MAELEZO imesema gazeti hilo lilishawahi kupewa onyo la maandishi tarehe 8 Mei 2026 kutokana na makosa kama hayo, ambapo liliagizwa kuimarisha weledi katika uhariri na kuhakikisha usahihi wa taarifa kabla ya kuzisambaza kwa umma
Hata hivyo, baada ya makosa hayo kujirudia miezi mitatu tu baada ya onyo hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Habari amesema alijiridhisha kuwa ni muhimu kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya gazeti hilo.
MAELEZO imeeleza kuwa kusitishwa kwa leseni hiyo kunaanza Agosti 19, 2026, na kunahusisha pia uzalishaji na usambazaji wa gazeti hilo kwa njia ya kielektroniki au mtandao. Aidha, MwanaHALISI ina haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa Waziri mwenye dhamana ya habari ndani ya siku 30.
Kwa hatua hiyo, MAELEZO imetoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuzingatia Sheria ya Huduma za Habari pamoja na misingi ya weledi katika uandishi na uhariri wa habari.