Latest Posts

WANANCHI NZEGA WALALAMIKIA FIDIA KUPISHA UJENZI WA KAMBI YA JESHI

Wananchi wa vitongoji vya Bugegelema, Mwakidomu, na Mwakabilu vilivyopo Kata ya Mbongwe, wilayani Nzega mkoani Tabora, wameonesha kutoridhishwa na mpango wa ulipaji wa fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa kambi ya Jeshi, wakidai kiwango kilichopangwa ni kidogo mno huku wakilalamikia mchakato huo kukosa ushirikishwaji wa kutosha.

Baadhi ya wananchi pamoja na viongozi wa maeneo hayo wamedai kuwa wamekuwa wakikabiliwa na vitisho kutoka kwa watu wanaofika maeneo yao wakiwa wamefunika nyuso zao, wakijitambulisha kama wanajeshi na kuwaagiza kuhama mara moja kabla hata ya kukamilisha taratibu za fidia.

Akitolea ufafanuzi malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai, amethibitisha kuwa Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa kambi hiyo ya Jeshi, akifafanua kuwa wananchi walihusishwa kikamilifu kupitia vikao mbalimbali vya uhamasishaji ambapo walipewa taarifa rasmi kuwa kiwango cha fidia ni Shilingi laki nane (800,000) kwa kila hekta.

Tukai amebainisha kuwa zoezi hilo limeshaanza kuchukua hatua kwani baadhi ya wananchi tayari wameshalipwa fedha zao na kuanza kuhama kwa hiari mara baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika.

Kuhusu madai ya wananchi kufanyiwa vitisho, Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa ofisi yake haijawahi kupokea taarifa au malalamiko yoyote rasmi ya aina hiyo, huku akiahidi kuwa Serikali itasimamia kwa karibu zoezi hilo ili kuhakikisha kila mwananchi anayestahili anapata haki yake kwa mujibu wa sheria kabla ya kupisha eneo hilo

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!