Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wa chama hicho nchi nzima kukutana mara kwa mara katika vikao rasmi vya kikatiba, ili kujadili masuala muhimu na kuepuka kupotoshwa na taarifa zisizo na ukweli zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Wasira ametoa wito huo tarehe 19 Agosti, 2026, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wakati akianza ziara rasmi ya kikazi ya kukagua uhai wa chama hicho na utekelezaji wa Ilani yake, ambapo amebainisha kuwa vikao hivyo vinawapa wanachama fursa ya kupata taarifa sahihi na kuambizana ukweli.
“Wanachama wetu nchi nzima, kwa mujibu wa Katiba mna vikao vya wanachama. Mkutane muambizane. Siku hizi kwenye mitandao kuna uongo mwingi sana. Usipoangalia unaweza hata wewe kushirikishwa kusema uongo,” amesema Wasira.

Amesisitiza kuwa pindi wanachama wanapokutana na kubaini kuwepo kwa madai au taarifa zinazotatiza zinazosambazwa mitandaoni, ni vyema wakawaalika watu wenye ujuzi na uelewa mpana ili wawasaidie kutoa ufafanuzi wa kina na sahihi wa kisheria au kiserikali.
“Kwa hiyo ni vizuri kukutana mkasema hili jambo limesemwa sana, maana yake ni nini? Mkamwita mtu anayejua akawasaidia kufafanua,” ameeleza.
Kuhusu misingi ya Taifa, Wasira amebainisha kuwa CCM itaendelea kulinda na kutetea urithi wa amani, uhuru, na umoja wa nchi uliopatikana kwa kazi kubwa na waasisi, akionya kuwa jitihada zote za kujaribu kubomoa msingi huo hazitafanikiwa.

“Hii ndiyo CCM. Kazi ya kwanza tulipewa ni uhuru na tunalinda. Ya pili ni umoja na tunahakikisha unabaki. Yeyote anayetaka kuubomoa anabomoa msingi ambao hawezi. Anaweza kutikisa matawi lakini mizizi itabaki chini,” amesema.
Ametamatisha kwa kurejelea wanaokosoa utendaji wa chama hicho kwa kudai kuwa hakijafanya chochote tangu kupatikana kwa uhuru, akieleza kuwa madai hayo ni ya kinyume cha ukweli na kwamba hata uhuru wa kujieleza unaotumiwa na wakosoaji hao ni matunda ya uongozi wa CCM.
“Wanasema hatujafanya chochote tangu uhuru. Lakini uhuru wa kusema ndio huo walionao. Mdomo una kazi mbili: kusema na kula. Mtu akisema hakuna chochote tangu uhuru, muache tu. Huyo ana matatizo anahitaji msaada,” amehitimisha Wasira.