Latest Posts

WASIRA AKEMEA VIONGOZI WASIO NA MSIMAMO CCM

 

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia haki kwa kutoegemea maslahi binafsi huku akikemea viongozi wasiokuwa na msimamo ndani ya CCM.

Wasira aliyasema hayo alipozungumza na viongozi pamoja na wanachama wa CCM wilayani Iramba mkoani Singida, leo (Agosti 20, 2026) ambapo aliwataka wanachama kufuata misingi inayozingatia haki katika uchaguzi wa viongozi ndani ya CCM.

“CCM inahitaji viongozi wenye msimamo katika mambo ya msingi na wasiobadilika kutokana na mazingira au maslahi binafsi. Tunataka uongozi ambao hayumbi. Tunataka mtu ambaye ana msimamo kwa mambo ya msingi. Huyo ndiye kiongozi wetu,” amesisitiza.

Alitoa wito kwa wanachama wa CCM kuhakikisha wanachagua viongozi kwa kuzingatia uwezo, uadilifu na misingi ya haki huku akionya dhidi ya viongozi wanaopatikana kwa rushwa.

Alisema CCM haipaswi kuruhusu uongozi unaotokana na rushwa, vitisho au ujanja wa aina yoyote kwa kuwa viongozi wanaochaguliwa ni kielelezo cha Chama katika jamii.

“Wanachama ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha watu wanaopewa dhamana ya kuongoza Chama wana sifa na uwezo unaohitajika. Sisi ndiyo tunateua wanachama. Msije mkakubali Chama chetu kikapata uongozi unaotokana na rushwa bila uwezo wa kuongoza,” alisema.

Alieleza kuwa viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wana majukumu ya kuwateua au kusimamia mchakato wa kupata viongozi wa chini yao, hivyo wanapaswa kuwa waangalifu katika maamuzi wanayofanya.

Wasira alisema wenyeviti wa wilaya wanahusika na uteuzi wa viongozi wa matawi, huku wenyeviti wa mikoa wakiwa na jukumu katika uteuzi wa viongozi ngazi ya kata.

Ameonya kiongozi atakayebainika kutumia nafasi yake vibaya kwa kupokea rushwa na kuteua viongozi wasio na uwezo, hatakiwi kuachwa bila kuwajibishwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!