Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Antiphas Lissu, imerejea tena mahakamani mchana wa Septemba 2, 2026, kwa ajili ya kusikiliza utetezi kutoka kwa Shahidi Namba Tatu wa upande wa utetezi, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Amani Golugwa.
Mshitakiwa Tundu Lissu mwenyewe ndiye aliyemuongoza Shahidi Golugwa katika kutoa ushahidi wake baada ya shahidi huyo kula kiapo kizimbani. Ushahidi wa Golugwa wa leo umejikita katika kueleza chimbuko la kampeni ya “No Reforms No Election”, kile alichokiita uozo uliotokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024, pamoja na ripoti za kimataifa zilizodai kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana (2025) haukuwa huru wala wa haki.
Golugwa ameeleza kuwa ndani ya CHADEMA, ameshika nafasi mbalimbali za uongozi kabla ya kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara tangu Januari 22, 2025. Miongoni mwa nafasi hizo ni Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa minne ya Tanga, Arusha, Manyara, na Kilimanjaro.
Golugwa amefafanua kuwa ili mwanachama wa CHADEMA apate nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu Bara, jina lake linapaswa kupendekezwa na Mwenyekiti wa chama mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Chama ambao ndio wanaothibitisha uteuzi huo baada ya kupitia wasifu na uwezo wake. Ameongeza kuwa majukumu yake kama Naibu Katibu Mkuu Bara ni pamoja na kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu, mwandishi wa kumbukumbu za vikao vya chama, na msimamizi mkuu wa itifaki katika vikao na mikutano ya chama.
Lissu alimsomea Golugwa maneno ya mashtaka yanayomkabili yanayodai kuwa tarehe 3 Aprili 2025 alitoa kauli kama vile “tutazuia uchaguzi” na “tutakinukisha”, akitaka kujua ushiriki wa shahidi kwenye mkutano huo.
Golugwa ameeleza kuwa anaufahamu mkutano huo vizuri sana na kuweka wazi kuwa haukupangwa wala kuandaliwa na Tundu Lissu kama mtu binafsi, bali uliandaliwa na Sekretarieti ya chama. Â Amesema wazo la kuitishwa kwa mkutano huo lilitoka kwa Katibu Mkuu (John Mnyika) aliyeleta mapendekezo kuwa kuna haja ya kukutana na “watia nia” ambao ni wadau muhimu wa chama.
Golugwa amebainisha kuwa sekretarieti ya chama ndiyo iliyofanya maandalizi yote ya kiutendaji ya mkutano huo wa ndani, akifafanua kuwa “watia nia” walioalikwa walikuwa ni wanachama wa CHADEMA waliogombea nafasi za udiwani, ubunge, au urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na bado walikuwa na nia ya kugombea tena mwaka 2025. Aidha, kulikuwa na watiania wapya (“freshers”) ambao walikuwa na nia ya kuingia kwenye michakato ya ndani ya CHADEMA ili kugombea nafasi hizo mnamo mwaka 2025.
Amesema kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuwaeleza na kuwafafanulia watia nia hao msimamo rasmi wa chama uliopitishwa na Mkutano Mkuu na kuazimiwa na Kamati Kuu, ambao ni msimamo wa “No Reforms No Election” (Bila Mabadiliko Hakuna Uchaguzi).
Akieleza chimbuko la msimamo wa “No Reforms No Election”, Golugwa amesema kuwa msimamo huo ulizaliwa baada ya kile alichokiita ukiukwaji mkubwa na uozo ulioshuhudiwa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mnamo Novemba 2024. Â Amesema Katibu Mkuu Mnyika alimtaka yeye (akiwa Katibu wa Kaskazini wakati huo) pamoja na makatibu wa kanda nyingine tisa kuwasilisha ripoti na maoni yao ya nini chama kifanye kufuatia uchaguzi huo.
Katika ripoti yake aliyomtumia Katibu Mkuu, Golugwa aliandika, “kwa ushenzi huu niliouona, chama kisishiriki uchaguzi mwingine wowote bila kushinikiza mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi”. Mapendekezo hayo yalichakatwa na Kamati Kuu na Desemba 10, 2024, aliyekuwa Mwenyekiti Freeman Mbowe alitangaza rasmi msimamo wa chama wa No Reforms No Election.
Aidha, Golugwa ameeleza kile alichokiita ushenzi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaosimamiwa na TAMISEMI ikiwamo ‘madudu’ kwenye uteuzi wa wagombea ambapo alieleza kuwa watumishi wa Tume ya Uchaguzi walikuwa wanajificha kwa makusudi na kufunga ofisi ili kukwepa kuwapa fomu wagombea wa upinzani, au kukataa kuzipokea pindi ziliporudishwa. Pia, amedai watumishi hao walishirikiana na wagombea wa CCM kuweka mapingamizi yasiyo na msingi, kama vile madai kuwa mgombea wa upinzani “hajui kusoma na kuandika” au “si mkazi wa eneo husika”, ili kuwaengua kwa makusudi.
Aidha, amesema kuwa kuhusu ‘madudu’kwenye Kampeni akieleza kuwa kampeni zilijaa vurugu zilizopangwa na kulindwa, na ratiba za kampeni zilitengenezwa kimkakati ili kuvibana na kuvionea vyama vya upinzani ikiwamo kuhamishia mikutano ya CHADEMA kwenye viwanja vilivyo mbali na makazi ya watu.
Aidha amebainisha uwepo wa hujuma dhidi ya mawakala akisema utaratibu unaelekeza kuwa mawakala wangekuta hati zao za kiapo kwenye vituo vya kura siku ya uchaguzi ili zitumike kama utambulisho wao. Hata hivyo, mawakala wa CHADEMA walipofika vituoni, wasimamizi wasaidizi waliwafukuza kwa madai kuwa viapo vyao havipo, huku mawakala wa CCM wakiwa wameshaingizwa ndani. Katika kipindi hicho mawakala wa CHADEMA walipokuwa nje, ndipo “ushenzi haswa wa wizi na uwekaji wa kura haramu” ulipofanyika.
Golugwa ameeleza matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa ya kushangaza akisema kuwa CCM ilitangazwa kushinda kwa asilimia 99.2 ya vijiji na mitaa yote nchini, huku vyama vyote vya upinzani vikiambulia asilimia 0.8 pekee. Katika Kanda yake ya Kaskazini, CCM ilitangazwa kushinda kwa asilimia 98.7.
Golugwa ameiambia mahakama kuwa kanuni zote za uendeshaji wa uchaguzi huo wa serikali za mitaa zilitungwa na Waziri wa TAMISEMI kwa wakati huo, Mohamed Mchengerwa, na wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi za halmashauri walikuwa ni Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ni wateule wa Rais moja kwa moja. Pia, wasimamizi katika ngazi za mitaa na vijiji walikuwa ni watendaji wa serikali.
Golugwa amesisitiza kuwa mambo yaleyale yaliyotokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, aliyashuhudia pia yakijirudia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na 2025. Amebainisha kuwa kadhia hii ya uenguaji wa wagombea inawapata wagombea wa CHADEMA, ACT Wazalendo, na CUF, lakini haijawahi kumkumba mgombea yeyote wa CCM katika nafasi yoyote ile tangu kuanzishwa kwa mfumo vya vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza wa 1995.
Lissu alimhoji Golugwa kuhusu ufahamu wake juu ya taarifa za waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka jana (2025). Golugwa amekiri kusoma ripoti za Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Ulaya (EU), na ripoti ya Taasisi ya Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki.
Akitolea mfano Ripoti ya Umoja wa Afrika (AU), Golugwa amesema ripoti hiyo ilisema wazi kuwa uchaguzi wa Tanzania haukuwa na viwango vya kidemokrasia na ulishuhudia wasimamizi wakiwaingizia wapiga kura kura nyingi ‘feki’ kwenye masanduku ya kura. Amesema AU ilihitimisha kuwa uchaguzi huo haukuwa na uadilifu wowote na haukufaa kabisa kuitwa uchaguzi.
Kutokana na muda wa mahakama kuisha, jopo la majaji limeahirishisha kesi hiyo hadi kesho asubuhi Septemba 3, 2026, ambapo utetezi wa Amani Golugwa unatarajiwa kuendelea mahakamani hapo kabla ya kuanza kwa maswali ya dodoso.