Latest Posts

ORYX GAS YATOA MITUNGI 600 NAMTUMBO, WANANCHI WAPIGWA MSASA MATUMIZI YA GESI

Kampuni ya Oryx Gas imekabidhi mitungi ya gesi 600 na vifaa vyake kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.

Oryx Gas imetoa mitungi hiyo ya gesi kwa wananchi hao kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria Juma Homera  kwa lengo la kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini ili kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Iman Mtafya,Meneja Fedha wa kampuni hiyo Ashery Mbasha amesema kupitia Uwezeshaji huo Oryx Gas inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

“Wilaya ya Namtumbo, kama ilivyo kwa maeneo mengi nchini Tanzania, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya matumizi makubwa ya kuni na mkaa. Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira.

“Hivyo kamahatua madhubuti hazitachukuliwa, vizazi vijavyo vinaweza kukumbana na uhaba mkubwa wa rasilimali za misitu na athari za mabadiliko ya tabianchi,”amesema na kuongeza kwa kutambua changamoto hiyo, Oryx Gas imeamua kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuhamasisha matumizi ya gesi ya LPG kama mbadala wa kuni na mkaa.

Amesisitiza matumizi ya gesi ya kupikia yatasaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza moshi majumbani, kuokoa muda wa kupika na kuongeza ubora wa maisha kwa ujumla.

Mbasha amesema dhamira ya Oryx Gas ni kuhakikisha Tanzania inafikia mabadiliko kamili ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Wilaya ya Namtumbo ni moja ya maeneo ambayo tumeyawekea kipaumbele katika safari hii muhimu.

“Oryx Gas pia imekuwa mshirika wa maendeleo katika wilaya hii ya Namtumbo kupitia miradi mbalimbali ya nishati safi. Miongoni mwa mafanikio hayo ni ufungaji wa mfumo wa hifadhi na usambazaji wa gesi ya LPG katika Shule ya Wasichana ya Samia Suluhu, hatua iliyowezesha taasisi hiyo kutumia nishati safi kwa manufaa ya wanafunzi na watumishi wake.”

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi wa Namtumbo hasa waliopata mitungi ya gesi ya Oryx kutumia majiko hayo kwa usalama na kuendelea kueneza elimu ya matumizi ya gesi ya LPG katika jamii zenu. Kwa pamoja tunaweza kujenga Namtumbo yenye mazingira bora, afya bora na maendeleo endelevu.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Namtumbo ,ambaye pia ni waziri wa Katiba na sheria Dk.Juma Homera ameishukuru kampuni ya Oryx kwa kuwapatia majiko 600 na Kati hayo majiko 215 yamekabidhiwa kwa wananchi wa Namtumbo na  mengine yatapelekwa na kugawanywa kila kata kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

Dk.Homera amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi ya kupikia amekuwa akisisitiza  utumiaji wa nishati safi hivyo amewataka wananchi kuunga mkono jitihada hizo za Rais na Serikali ya Awamu ya Sita kwa vitendo huku akiipongeza Oryx gas kwa ushirikiano  ambao wamekuwa wakiutoa kwa wananchi wa Namtumbo.

Kwa upande wake Mama Lishe Anifa Mahela amepongeza mpango huo mzuri wa kutoa elimu na kugawa bure mitungi kwa wajasiriamali huku akiiomba Serikali na wadau kama Oryx kuwasaidia kupata mitungi ya gesi na majiko ya nishati safi kwa bei ya ruzuku kutokana na mtaji mdogo walionao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!