Latest Posts

WAWEKEZAJI WA JAPAN WAHAMASISHWA KUWEKEZA SEKTA YA VIWANDA TANZANIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea na juhudi zake za kuongeza kiwango cha uwekezaji kutoka nje kwa kuishawishi Serikali ya Japan na sekta yake binafsi kuongeza uwekezaji nchini ili kusaidia kufikia lengo kubwa la kihistoria la kukuza uchumi wa nchi kufikia Dola za Kimarekani Trilioni moja ($1 trillion) ifikapo mwaka 2050.

Wito huo umetolewa Jumanne, Septemba 8, 2026, jijini Tokyo, Japan, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, wakati wa mazungumzo yake maalum na Naibu Waziri wa Bunge wa Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan (METI), Komori Takuo.

Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Tanzania imeanza awamu mpya ya mageuzi ya kiuchumi inayongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31. Amesisitiza kuwa kufikia malengo hayo makubwa kunahitaji washirika thabiti wa kimkakati kama Japan, nchi yenye teknolojia ya kisasa, ujuzi wa viwanda, na uwezo mkubwa wa usimamizi wa ubora

Akizungumzia mwelekeo mpya wa ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili, Prof. Mkumbo amesema, “Ushahidi wetu ni rahisi: tunataka kuhama kutoka kwenye biashara kwenda kwenye uwekezaji, kutoka uwekezaji kwenda kwenye viwanda, na kutoka kwenye kusafirisha malighafi ghafi kwenda kwenye uzalishaji unaoongeza thamani”.

Waziri Mkumbo amebainisha sekta muhimu ambazo kampuni za Kijapan zinaweza kuwekeza ili kupata soko kubwa la Tanzania pamoja na masoko ya kikanda ya EAC, SADC, na soko huru la Afrika (AfCFTA). Sekta hizo ni pamoja na sekta ya magari hasa kuunganisha magari, pikipiki, zana za kilimo, vipuri, betri, na mifumo ya usafiri wa umeme.

Sekta nyingine ni uwekezaji katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba kupitia eneo maalum la uwekezaji wa dawa (Pharmaceutical Special Economic Zone) huko Bagamoyo, ushiriki katika mradi mkubwa wa chuma wa Liganga-Mchuchuma, pamoja na mifumo ya kisasa ya kilimo, umwagiliaji, usafirishaji, na uhifadhi wa baridi, uchakataji wa madini ya grafaiti, nikeli, kobalti na lithium ili kuongeza thamani yake kabla ya kusafirishwa nje, na uwekezaji katika miundombinu na usafirishaji hasa kwenye reli ya SGR, bandari, uchumi wa buluu, na ujenzi wa miji ya kisasa.

Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa uwekezaji unaotafutwa na Tanzania ni ule unaosaidia kukuza uwezo wa ndani na kutengeneza fursa za kiuchumi kwa wananchi:  “Kwa Tanzania, uwekezaji sio mwisho wa jambo lenyewe. Tunatafuta uwekezaji unaotengeneza kazi zenye tija, unaoendeleza ujuzi, unaohamisha teknolojia, unaoimarisha biashara za ndani na kuziingiza kampuni za Kitanzania kwenye minyororo ya thamani ya kikanda na kimataifa.”

Waziri Mkumbo ameiomba METI kusaidia katika kuhamasisha wawekezaji na taasisi za kifedha za Japan kuchangamkia fursa zilizopo Tanzania, kusaidia katika uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, pamoja na kuimarisha majukwaa ya majadiliano kati ya serikali na wafanyabiashara (G2B na B2B) ili kupata miradi thabiti inayoweza kufadhiliwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!