Latest Posts

ANAYETUHUMIWA KUMKATA SCOLA VIGANJA VYOTE VYA MIKONO AKAMATWA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limefanikiwa kumkamata Emmanuel Elisante Mariki (28), mkazi wa Kijiji cha Lyasongoro, Kata ya Marangu Mashariki, Wilaya ya Moshi, aliyekuwa akitafutwa kwa tuhuma za kuwashambulia na kuwajeruhi vibaya watu wawili kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Tukio hilo la kikatili lilitokea mnamo Agosti 24, 2026, majira ya saa kumi na nusu alfajiri, ambapo mtuhumiwa huyo alimshambulia Scola Bernad (23) pamoja na mtoto wake, Kelvin Baraka mwenye umri wa miaka miwili, na kuwajeruhi sehemu mbalimbali za miili yao huku Scola akikatwa na kutenganishwa viganja vya mikono yake kabla ya mtuhumiwa kutokomea.

Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi uliobainishwa kupitia taarifa ya Agosti 25, 2026, ulionyesha kuwa chanzo cha tukio hilo kinatajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kukuta jumbe za kimapenzi kutoka kwa mwanaume mwingine kwenye simu ya Scola, huku taarifa za ndani zikieleza kuwa wawili hao waliwahi kugombana awali na kusababisha mtuhumiwa kuondolewa kazini walipokuwa wakifanya kazi za ndani.

Akithibitisha kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema kuwa kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianzisha msako mkali kwa kushirikiana na wananchi, hatua iliyowezesha kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo Septemba 13, 2026, majira ya saa sita mchana, alipokuwa amejificha eneo la Bonite Shirimatunda, Wilaya ya Moshi.

Kamanda Maigwa ameeleza kuwa kwa sasa mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya taratibu za uchunguzi na hatua za kisheria, na atafikishwa mahakamani mara tu taratibu hizo zitakapokamilika.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao uliosaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo, na limewasisitiza kuendelea kutoa taarifa za siri kuhusu wahalifu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!