Kundi la EPP (The EPP Group), ambalo ni kundi kubwa na lenye nguvu zaidi la kisiasa ndani ya Bunge la Umoja wa Ulaya, limependekeza rasmi jina la mwanasiasa, wakili, na mwanaharakati wa haki za binadamu wa Tanzania, Tundu Antiphas Lissu, kuwania Tuzo ya Sakharov ya mwaka 2026 (Sakharov Prize for Freedom of Thought).
Tuzo hiyo ya Uhuru wa Kujieleza ndiyo heshima ya juu zaidi inayotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kutambua watu binafsi, vikundi, au mashirika yaliyojitolea maisha yao kutetea haki za binadamu, uhuru wa kujieleza, demokrasia, na utawala wa sheria.
Katika taarifa yake rasmi iliyotolewa kupitia mtandao wa X, kundi la EPP limeweka wazi sababu za kumteua Lissu likisema, “baada ya kunusurika katika jaribio la mauaji la mwaka 2017, Lissu alirejea Tanzania kuendelea kupigania mabadiliko ya kidemokrasia, lakini akakumbana na ukamataji, mashtaka ya uhaini na hakushiriki katika uchaguzi wa Urais wa mwaka 2025, huku chama chake kikizuiwa kushiriki. Kesi yake inaakisi mmomonyoko mpana wa mfumo wa vyama vingi vya kidemokrasia na ushindani wa kisiasa nchini Tanzania”.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa Lissu anawakilisha muunganiko thabiti wa ujasiri binafsi, msimamo wa kidemokrasia na umuhimu wa siasa za dunia. Kuteuliwa kwake kunathibitisha kuwa Ulaya inasimama na wale wanaotetea demokrasia ya kikatiba na uhuru wa kisiasa barani Afrika na katika nchi zingine washirika wa EU. Bw. Lissu ni kielelezo halisi cha utetezi wa demokrasia, siasa za vyama vingi, utawala wa sheria na uhuru wa kimsingi kwa gharama kubwa sana za maisha yake binafsi.
Kutokana na taarifa hiyo, Mjumbe wa Bunge la Ulaya, David McAllister, ameeleza kuwa Lissu amekuwa kizuizini kwa zaidi ya siku 500 kwasababu ya kupigania uchaguzi huru na wa haki pamoja na mustakabali wa kidemokrasia wa nchi yake.
“Hakuna shaka yoyote kuhusu asili ya kisiasa ya kuzuiliwa kwake. Ni mfano wa wazi wa shinikizo linaloongezeka dhidi ya upinzani, maandamano ya amani na uhuru wa kisiasa nchini Tanzania”, ameeleza McAllister.
McAllister ameongeza kuwa licha ya kile alichokiita mateso na ukandamizaji, Lissu amesalia imara katika msimamo wake wa kidemokrasia na kwamba kuteuliwa kwake kuwania tuzo hiyo kunaheshimu ujasiri huo wa kipekee.
Baada ya kuteuliwa kuwania Tuzo ya Sakharov, uteuzi wa mtu husika hupitia hatua kadhaa za tathmini na mchujo ndani ya Bunge la Ulaya (European Parliament) ikiwamo kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Maendeleo kuufanya kikao cha pamoja ili kufanya tathmini ya wagombea wote walioteuliwa. Kamati hizi mbili hupiga kura na kuchagua orodha fupi ya wateuliwa watatu walioingia hatua ya fainali. Baada ya hapo, Mkutano wa Marais ambao unajumuisha Rais wa Bunge la Ulaya na viongozi wa vikundi vya kisiasa hukutana na kumchagua mshindi wa mwisho (laureate).
Mshindi wa Tuzo ya Sakharov hukabidhiwa cheti cha heshima pamoja na zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Euro 50,000 (sawa na zaidi ya Shilingi milioni 150 za Kitanzania). Hafla ya utoaji wa tuzo hii hufanyika mwezi Desemba kila mwaka katika ofisi za Bunge la Ulaya jijini Strasbourg, nchini Ufaransa.
Baada ya hapo mshindi hujiunga na Mtandao wa Tuzo ya Sakharov (Sakharov Prize Network) ambao huwasaidia kuwasiliana, kushirikiana, na kuwalinda washindi wanaokabiliwa na hatari au vitisho katika nchi zao. Washindi huendelea kufanya kazi kama mabalozi wa kutetea haki za binadamu na uhuru wa fikra duniani kote, wakishirikiana kwa karibu na Bunge la Ulaya.
Watu wengi waliowahi kushinda tuzo hii ni wale waliopitia mateso, vifungo, au hatari kubwa kwa ajili ya misimamo yao ya kutetea haki. Baadhi ya waliowahi kutunukiwa tuzo hii huko nyuma ni pamoja na Nelson Mandela, na mwanaharakati wa Urusi Anatoly Marchenko ambao ni washindi wa kwanza kabisa mwaka 1988. Kofi Annan na wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa mwaka 2003), na Malala Yousafzai, mwanaharakati wa elimu kwa watoto wa kike kutoka Pakistan mwaka 2013.