Latest Posts

WAZIRI KATAMBI AAGIZA POLISI KUMSAKA DUDUBAYA, MWENYEWE ASEMA, “MSIHANGAIKE, NAKUJA MWENYEWE”

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria msanii Godfrey Tumaini maarufu Dudubaya, baada ya kushindwa kuitikia wito wa Wizara hiyo.

Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa, Katambi amesema Dudubaya alikuwa ametakiwa kufika Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya kutajwa katika tuhuma za makosa ya jinai, lakini licha ya kuitwa kwa mara ya pili, bado hakufika.

Waziri amesema Dudubaya ameonekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa kauli ambayo Waziri ameielezea kuwa ni kukaidi wito wa Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Katambi ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha Dudubaya anapatikana kokote aliko na kufikishwa mbele ya Jeshi hilo ili achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Waziri Katambi amesema kutokana na mwenendo wa Dudubaya na tuhuma zinazomkabili, ameagiza pia kufanyike vipimo vinavyohitajika ili kubaini hali yake, na taarifa kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali itakapopatikana, hatua zaidi zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Dudubaya amejibu agizo la kukamatwa kwake kwa kutangaza kuwa anaenda kujisalimisha mwenyewe katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police Station) jijini Dar es Salaam

Kupitia video aliyoichapisha kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Instagram mara baada ya kupokea taarifa za kusakwa kwake, Dudubaya amekiri kulipata tamko la Waziri Katambi lililoagiza akamatwe

Hata hivyo, msanii huyo ameweka wazi kuwa yeye si mtu wa kukimbia mkono wa sheria. Amefafanua kuwa amekuwa na urafiki wa karibu na wa muda mrefu na Jeshi la Polisi tangu alipoanza tasnia ya muziki, akibainisha kuwa mwanamuziki yeyote hawezi kufanya tamasha la hadhara bila kupata ulinzi thabiti wa askari polisi.

“Mimi ni Mtanzania. Mimi siwezi kukimbia polisi,” amesema Dudubaya katika video hiyo akisisitiza uzalendo wake

Katika kujitetea dhidi ya tuhuma zilizopo nyuma ya wito wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Dudubaya amesema hana hatia ya makosa makubwa ya kijinai yanayoweza kumfanya ajifiche au kukimbia mamlaka za usalama nchini. Amesisitiza kuwa yeye si gaidi, si muuaji, si muuzaji wa dawa za kulevya, na wala si mbakaji, na kwamba hana tuhuma zozote zinazofanana na makosa hayo mazito ya jinai

kuondoa usumbufu kwa vyombo vya dola, msanii huyo amewataka polisi kutosumbuka au kupoteza nguvu katika kumtafuta kwani anafanya maamuzi ya kwenda mwenyewe kituoni. Alitangaza kuwa anaondoka moja kwa moja kutoka nyumbani kwake eneo la Bahari Beach, jijini Dar es Salaam, kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi kukabiliana na wito huo

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!