Diwani wa Kata ya Kalangalala katika Manispaa ya Geita ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Reuben Sagayika, amehitimu mafunzo ya utawala, uongozi na maendeleo yaliyoandaliwa na Serikali ya China na kuwashirikisha washiriki kutoka nchi 23 za ukanda wa Bahari ya Hindi.
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa takribani wiki tatu, yamefanyika katika Yunnan International Center for Economic and Technical Exchange jijini Kunming, China, na kuratibiwa na Wizara ya Biashara ya Jamhuri ya Watu wa China.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti cha kuhitimu mafunzo hayo, Sagayika amesema amepata fursa ya kujifunza namna China inavyotumia mifumo bora ya utawala, uongozi na mipango ya muda mrefu katika kuchochea maendeleo ya wananchi.
Amesema miongoni mwa mambo aliyojifunza ni umuhimu wa kuwa na uongozi madhubuti, nidhamu na uwajibikaji, pamoja na kuwa na maono ya muda mrefu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Sagayika amesema pia amejifunza umuhimu wa kuimarisha taasisi za serikali, kuwekeza katika viwanda, miundombinu, teknolojia na rasilimali watu, akibainisha kuwa maendeleo ya vijijini ni sehemu muhimu katika kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi.

Kwa upande wa Tanzania, Sagayika amesema uzoefu alioupata nchini China unaweza kutumika kama fursa ya kuboresha mifumo ya maendeleo kwa kuzingatia mazingira, uwezo na mahitaji ya Tanzania.
Aidha, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na China unaendelea kuwa na umuhimu katika kutoa fursa za biashara, uwekezaji, teknolojia pamoja na ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu.
Sagayika amesema atashirikisha maarifa na uzoefu alioupata katika mafunzo hayo na wadau mbalimbali nchini, ili yaweze kuchangia katika kuboresha utawala, uongozi na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
