Latest Posts

PM AAGIZA VIPANDE VYOTE VYA SGR KUKAMILIKA KUFUNGUA UCHUMI

Serikali ya Tanzania imetoa agizo thabiti kwa Wizara ya Uchukuzi, Shirika la Reli Tanzania (TRC), na wakandarasi kuweka mikakati mahususi na kupambana usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katika vipande vyote unakamilika kwa kasi.

Agizo hilo limetolewa leo Ijumaa, Septemba 4, 2026, bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha hoja ya kuahirisha Bunge la 13, Mkutano wa Nne. Dkt. Mwigulu ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akilihutubia Bunge, alibainisha wazi dhamira yake ya dhati ya kukamilisha miradi yote ya kimkakati nchini.

“Naziagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi, zikishirikiana na Shirika la Reli, wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga vipande hivi vya miradi ya Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na wale waliopewa jukumu la kuhamasisha fedha za miradi hiyo, kupambana usiku na mchana”, ameeleza.

Dkt. Mwigulu amefafanua kuwa dhamira ya Rais Samia imedhihirishwa kwa vitendo kupitia falsafa yake ya “continuity and change” (mwendelezo na mabadiliko) ambapo falsafa hii imeshuhudia kukamilika kwa baadhi ya miradi mikubwa ya kielelezo nchini, ikiwemo mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema chini ya falsafa hiyo hiyo, serikali imejikita katika kukamilisha ujenzi wa miradi ya kielelezo kama reli ya SGR kwa vipande vyote, huku mfano wa karibuni ukiwa ni uzinduzi wa kipande cha kutoka Tabora hadi Kigoma uliofanywa na Rais Samia.

 

Hatua za Utekelezaji wa Vipande vya SGR.

Waziri Mkuu ametoa mchanganuo wa hatua za ujenzi kwa vipande tofauti vya reli hiyo nchini:

Kipande cha Isaka hadi Mwanza: Kiko katika hatua nzuri ya utekelezaji na kuanzia sasa hadi kufikia Desemba 2026, kinatarajiwa kuwa katika hatua ya ukamilishaji.

Vipande vya Isaka–Tabora na Makutupora–Tabora: Vipande hivi vyote viwili bado viko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ili kufanikisha azma ya kukamilisha vipande hivyo pamoja na kile cha Makutupora hadi Dodoma, Dkt. Mwigulu ameelekeza Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na TRC kuweka mkakati madhubuti wa kuongeza kasi ya ujenzi.

 

Shabaha ya Safari ya Dodoma Ifikapo 2030.

Dkt. Mwigulu ameweka malengo makubwa ya kisiasa na kiuchumi kuelekea mwaka 2030, akitaka wajumbe na wananchi kusafiri kwa urahisi kwa kutumia miundombinu hiyo ya kisasa:

“Ikiwezekana mheshimiwa spika ifikapo 2030 wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wa kutoka Mwanza, Mara, Shinyanga, Geita, waje Dodoma wakiwa wamepanda SGR ya kutoka Mwanza mpaka hapa Dodoma,” alisema Dkt. Mwigulu.

Aliongeza kuwa, kutokana na uzoefu uliopatikana katika ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na vipande vingine vya reli, lengo hilo linawezekana kabisa. Alibainisha kuwa hata wajumbe kutoka mikoa ya Rukwa, Katavi, na Kigoma nao wanaweza kuanza safari zao kwa kukamata reli hiyo katika kituo cha Tabora kuelekea Dodoma

Waziri Mkuu amehitimisha kwa kuahidi kuwa, mara baada ya taratibu za utekelezaji kukamilika, atakutana na Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi, wakandarasi, pamoja na timu iliyopewa jukumu la kuhamasisha fedha za miradi ili “kukimbia” kwa pamoja na kukamilisha mradi huo kwa ajili ya kufungua uchumi wa nchi

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!