Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Godbless Lema ametangaza kughairi kuzungumza na waandishi wa habari kama alivyokuwa amepanga kufanya leo majira ya saa sita mchana.
Jana Septemba 15, 2026 Lema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii alitangaza kuwa angefanya mkutano huo ambao ulilenga kufafanua tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kwa siku kadhaa.
“Mkutano wangu na waandishi wa habari niliokuwa nifanye katika Hotel ya Golden Tulip nimeuahirisha. Nimesikiliza hotuba za Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Wameeleza vizuri kuhusu uvumi na upotoshaji uliokuwa ukifanyika juu yangu na misimamo juu ya chama chetu. Nimedumu katika mapambano haya kwa zaidi ya miaka 22. Nimeenda lock-up zaidi ya mara 50. Nimezunguka nchi hii usiku na zaidi ya mara tatu. Nimewahi kuwa magerezani mara kadhaa, nimekoswa kuuawa zaidi ya mara tatu, na nimewahi kukimbia nchi. Katika yote haya, nimekuwa nikitoa sadaka kubwa kwa ajili ya mapambano haya, ikiwemo ku-sacrifice familia yangu mara zote. Kazi hii kwangu si ajira, si cheo, wala si njia ya kujitafutia maslahi. Ni huduma. Ni wito. Ni kama injili ninayoamini na kuitumikia. Kwa hiyo, siwezi kuruhusu uvumi, upotoshaji au tafsiri za watu kuniondoa kwenye misingi ambayo nimeisimamia kwa zaidi ya miongo miwili. Nitakuwa kwenye mapambano haya kwa imani, ujasiri na dhamira njema siku zote”.
Kuahirishwa kwa mkutano huu kunakuja katikati ya mjadala mzito ulioibuka nchini kufuatia kifo cha mume wa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Marehemu Hafidh Ameir Hassan, aliyefariki dunia Septemba 7, 2026, katika Hospitali ya Emilio Mzena na kuzikwa siku hiyo hiyo huko Kizimkazi, Zanzibar.
Wakati vyama vingine vya siasa vikienda msibani na kumfariji Rais Samia, viongozi wa CHADEMA hawakuonekana msibani wala chama kutoa taarifa rasmi ya rambirambi. Hata hivyo, Septemba 7, 2026, Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini na kukaa mahabusu kwa takribani mwaka mmoja na miezi sita, alisikika akiwaambia viongozi wake Mahakama Kuu Dar es Salaam: “Nasikia kuna msiba, wape pole… jamani pelekeni pole zangu kwa wafiwa”.
Septemba 11, 2026, kabla ya kesi yake kuanza, Lissu alisikika akirejea salamu hizo na kuhoji kama zimefika alipomuuliza Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Mzee: “Makamu umepeleka rambirambi zangu bwana?”, na alipojibiwa kuwa zimefika, Lissu aliongeza: “Nimefurahi kama zimefika
Septemba 13, 2026, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kuwasilisha salamu alizozitaja kuwa ni za Lissu na zake mwenyewe, jambo ambalo liliwawasha baadhi ya wanaharakati na wafuasi wa mtandaoni waliomshambulia Lema kwa matusi na kumwita msaliti. Wapo waliohoji ni kwanini ampe pole Rais wakati kuna watu walikufa au kuumizwa bila kupewa pole huku wengine wakidai kuwa hakuna mahali Lissu alipoashiria salamu na pole zake zilimlenga Dkt. Samia. Hata hivyo, baadhi ya wananchi walimuunga mkono Lema na Lissu kwa kile walichokiita kuonesha ukomavu wa hali ya juu.
Akijibu mashambulizi hayo Septemba 14, 2026, Lema amesisitiza kuwa hatua ya Lissu kutoa rambirambi si unyonge bali ni hekima na ukomavu akiandika, “Nimeona matusi na sintofahamu nyingi mtandaoni baada ya kuchapisha ujumbe wa kutoa pole kwa Mama Samia, hasa niliponukuu salamu za pole za Mwenyekiti Lissu kutoka gerezani. Kwa sisi jamii tunaodai kupigania uhuru wa maoni na demokrasia, hili linapaswa kutufikirisha. Kutofautiana kwa hoja hakuhitaji matusi, dhihaka wala chuki”.
Licha ya kujibu mashambulizi hayo, watumiaji mbalimbali wa mitandao ya kijamii ambao wengine ni wanaharakati waliendelea kumshambulia Lema wengine wakidai kuwa amenunuliwa na anatumika na kundi Fulani la watu kuididimiza na kuiharibu CHADEMA na viongozi wake waandamizi, na hivyo Lema akawa amedhamiria kuitisha mkutano na wanahabari.