
SERIKALI ya Mkoa wa Dar es Salaam imeweka wazi mipango na mikakati yake ya kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2028 pamoja na uboreshaji wa mazingira ya wafanyabiashara wadogo jijini humo.
Akizungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Septemba 17, 2026 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amebainisha kuwa, mkoa umejipanga kikamilifu kukabiliana na mfumo wa ‘Double Cohort’ utakaoshuhudia wanafunzi wa Darasa la Sita na la saba wakihitimu na kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa pamoja mwaka 2028.
Chalamila ameeleza kuwa serikali ya mkoa inafanya tathmini na ujenzi wa miundombinu mipya ya shule ili kuhakikisha madarasa na vifaa vya kujifunzia vinatosheleza na hakuna mwanafunzi atakayekosa nafasi.
Kuhusu usimamizi wa biashara, Chalamila amesema mkoa unatekeleza mpango wa kuwapanga wafanyabiashara wadogo na machinga ili kuondoa kero ya biashara kufanyika kando ya barabara, juu ya mifereji na maeneo yasiyorasmi.
Ameeleza kuwa wameanza na kampeni ya kutoa elimu kwa wiki mbili ili kuwahimiza kurejea kwenye masoko rasmi bila kutumia nguvu, huku wakishirikiana na sekta binafsi kupunguza kodi za fremu na kuongeza nafasi mpya za biashara.
Pia, Chalamila amesisitiza kuwa, wafanyabiashara wote walioko ndani ya maeneo rasmi kama lango la soko la Kariakoo watafanya biashara kulingana na taratibu zilizowekwa, ikiwa ni pamoja na kuweka miongozo thabiti ya kutenganisha biashara za wazalendo na zile za raia wa kigeni wanaofanya biashara za rejareja au umachinga.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wananchi, wazazi, na wafanyabiashara kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa mipango hiyo ili kuleta nidhamu ya kibiashara, kuimarisha sekta ya elimu, na kuendeleza miundombinu ya jiji la Dar es Salaam.