Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezidisha msako na udhibiti dhidi ya vitendo vya ukwepaji kodi, biashara za magendo na ukiukaji wa maadili, ambapo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita imekamilisha uchunguzi wa mashauri 130 ya ukwepaji kodi yenye thamani ya Shilingi bilioni 331.15 na kukusanya Shilingi bilioni 44.74.
Katika taarifa yake ya utendaji kazi ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 (Julai – Septemba 2026), Mamlaka hiyo imeweka wazi kuwa haitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu dhidi ya mianya yote inayoisababishia Serikali hasara, ikijumuisha wafanyabiashara wasio waaminifu na watumishi wa umma wanaokiuka misingi ya kazi.
Katika udhibiti wa mpakani, TRA imefanya operesheni 1,185 za kufuatilia uingizaji wa mizigo kwa njia zisizorasmi (magendo), ambapo ilikamata bidhaa za magendo zenye thamani ya Shilingi bilioni 12.72 na kufanikiwa kuokoa kodi ya Shilingi bilioni 5.34. Hali kadhalika, kuzuia mizigo na magari 47,773 yanayohusika na usafirishaji wa mizigo, kulibaini makosa 197 ya udanganyifu na kuiwezesha TRA kukusanya Shilingi bilioni 79.68
Akitangaza hatua zilizochukuliwa kuimarisha nidhamu na uwajibikaji ndani ya taasisi hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, kupitia taarifa rasmi amesema, “TRA imewapatia mafunzo watumishi 1,028 ili kuboresha ujuzi wao katika usimamizi wa sheria za kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Aidha, imeimarisha maadili ya watumishi kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 09 waliobainika kuwa na changamoto mbalimbali za kimaadili katika kipindi husika”.
Mbali na hatua hizo za kinidhamu na udhibiti wa mpakani, Mamlaka hiyo imefanikiwa pia kutatua mashauri 10 ya migogoro ya kodi mahakamani yenye thamani ya Shilingi bilioni 7.78, hatua iliyotajwa kuongeza usawa na kuweka mazingira salama ya biashara na uwekezaji nchini
Kwa ujumla, TRA imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi trilioni 10.65 kwa kipindi hicho sawa na ufanisi wa asilimia 107.49 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni 9.91. Makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 18.81, ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 8.96 yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2025/26.
Mwenda amesema TRA imeimarisha utoaji wa huduma kwa walipakodi kwa kuboresha mifumo, mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili kurahisha na kuchochea ulipaji kodi wa hiyari.
Katika hatua nyingine, sehemu ya makusanyo kwenye Pato la Taifa kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27 imefikia asilimia 15.80, ukilinganisha na asilimia 12.7 iliyofikiwa mwaka 2021/22 wakati Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipoingia madarakani. Makusanyo haya ni wastani wa makusanyo ya Shilingi trilioni 3.55 kwa mwezi kutoka wastani wa Shilingi Trilioni 2.98.
Katika kipindi cha robo ya kwanza (Julai -Septemba) mwaka wa fedha 2026/27, TRA imesajili walipakodi wapya 447,611 na kupelekea idadi ya walipakodi kufikia 9,011,783, ukilinganisha na walipakodi 8,564,172 waliokuwa wamesajiliwa mpaka mwezi Juni 2026.
Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa ufanisi wa watumishi wa TRA, matumizi ya ofisi inayotembea (mobile vehicle office), matumizi ya vishikwambi katika kuwatembelea wateja walioko maeneo ya pembezoni, pamoja na ufunguzi wa ofisi mpya katika maeneo mbalimbali nchini.

