Waziri wa Mifugo na Uvuvi Nchini Tanzania Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewataka wataalamu wa mifugo na uvuvi nchini kuboresha utendaji kwa kuzingatia sayansi, weledi na maadili ya taaluma ili kutoa huduma bora kwa wafugaji na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Akifungua Kongamano la 49 la Kitaaluma na Mkutano Mkuu wa 50 wa Chama cha Wataalamu wa Mifugo Tanzania (TSAP), mkoani Iringa, Dkt. Kakurwa amesema malalamiko kuhusu huduma zinazotolewa na baadhi ya wataalamu yanapaswa kuwaamsha kujitathmini, kuwajibika na kurejesha imani ya wafugaji.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha Tanzania inafikia utoshelevu wa protini itokanayo na nyama, maziwa, mayai na samaki kabla ya mwaka 2050, Ili kufikia lengo hilo, amesisitiza kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa bidhaa na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Aidha, ameitaka TSAP kuimarisha weledi wa wanachama wake na kuhimiza matumizi ya tafiti, teknolojia na ubunifu katika kuboresha afya na lishe ya mifugo, uhifadhi wa malisho na uzalishaji huku akiwataka wataalamu kujifunza uzoefu wa Iringa katika tasnia ya maziwa na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TSAP, Dkt. Zabron Nziku, ameiomba Serikali kuimarisha ushirikiano na chama hicho ili matokeo ya tafiti yatumike kuboresha sera na kutatua changamoto za wafugaji akiesema chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1973 kina takribani wanachama 1,000, huku maandalizi ya kuanzisha jarida la kisayansi yakifikia asilimia 85.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amewataka wataalamu kuelekeza tafiti katika kutatua changamoto za wafugaji, ikiwamo kudhoofika kwa mifugo na matumizi ya mbinu za jadi.
Akipigilia msumari hoja hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Madele, amesema Serikali inataka tafiti na ubunifu viunge mkono maendeleo ya sekta hizo kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kwa upande wa sekta binafsi, Mkurugenzi wa ASAS, Fuad Abri, amesisitiza umuhimu wa tafiti na utaalamu katika kukuza sekta ya mifugo na uchumi wa taifa, huku akiahidi kuendelea kuwaunga mkono wataalamu.
