Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imebaini mapungufu mbalimbali katika utekelezaji wa miradi 14 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 81, ukiwamo mradi mkubwa wa ujenzi wa viwanja vitatu vya mazoezi vinavyoandaliwa kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imetolewa leo, Jumatano, Novemba 11, 2026, na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Kinondoni, Bi. Elizabeth Mokiwa, wakati akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi na mafanikio ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi sita (Aprili hadi Septemba 2026) mbele ya vyombo vya habari
Kwa mujibu wa Mwananchi, Bi. Mokiwa ameeleza kuwa mradi huo wa Sekta ya Michezo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 51.6 unajumuisha ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Leaders Club, Gymkhana 2, na Uwanja wa Farasi.
“Katika kutekeleza jukumu letu tumebaini mapungufu kadhaa katika utekelezaji wa miradi hiyo na hivyo kufanya vikao kazi na watekelezaji wakiwemo wakandarasi, washauri, wasimamizi, na Ofisi ya Mthibiti Ubora ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa,” amesema Bi. Mokiwa, huku akibainisha kuwa baadhi ya mapungufu tayari yameshafanyiwa kazi na mengine yanaendelea kurekebishwa.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Kinondoni imeeleza kuwa katika kipindi hicho ilipokea jumla ya malalamiko 110, ambapo malalamiko 47 yalihusu makosa ya rushwa na yanaendelea kuchunguzwa katika hatua mbalimbali, huku walalamikaji wa mashauri 63 yasiyohusu rushwa wakipewa ushauri wa kisheria.
Aidha, katika eneo la uendeshaji wa mashtaka, kesi 14 zilikuwa zikiendelea mahakamani (ikiwemo kesi mpya 10 zilizofunguliwa). Katika mashauri 12 yaliyotolewa maamuzi na mahakama katika kipindi hicho, Jamhuri ilifanikiwa kushinda kesi 9.
Bi. Mokiwa ameongeza kuwa TAKUKURU ilifanikiwa kuokoa Shilingi milioni 37 za ushuru na adhabu zilizolipwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatia oparesheni iliyofanyika katika Pwani ya Kunduchi, ambapo gari lililokuwa limesafirisha magendo ya madumu 510 ya mafuta ya kula (lita 20 kila moja) bila kulipa kodi lilinaswa.
Baada ya mamlaka husika kujiridhisha kuwa mafuta hayo ni salama kwa matumizi ya binadamu na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mwagizaji na mmiliki wa gari, ushuru na faini vililipwa kabla ya bidhaa hizo kuruhusiwa. TAKUKURU imetoa wito kwa wafanyabiashara kufuata sheria za uingizaji wa bidhaa nchini ili kulinda afya za wananchi, ushindani wa haki, na uchumi wa Taifa.