Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Angelina Marco amewasihi wazee wa mila kutoka koo mbalimbali wilayani humo zikiwemo koo za Watimbaru, Wakira, Wanyabasi, na Warenchoka kutoa tamko kali la kuzuia na kupiga marufuku vitendo vya ukeketaji, ambavyo vimekuwa vikitolewa hofu ya kufanyika kwa siri pindi shule zitakapofungwa kwa ajili ya likizo.
Angelina alitoa ombi hilo nyeti Novemba 10, 2026, alipokuwa akizungumza na wazee hao wa mila katika Kijiji cha Rung’abure, wilayani humo, akiwataka kuungana na Serikali kulinda mustakabali wa mtoto wa kike dhidi ya ukatili huo unaoathiri afya na elimu yao.

“Niwaombe sana wazee wangu, katika hili niko chini ya miguu yenu; tusaidieni kutoa kauli. Najua nyinyi mkizungumza kauli yenu inatekelezwa. Katika hili hatuhitaji watoto wetu wa kike wakeketwe, tuwaache wasome kwa ajili ya mustakabali wa kesho yao, hawa ni msaada kwenu kesho,” amesema Angelina Marco.
Kwa upande wao, wazee wa mila waliohudhuria kikao hicho wamepokea ombi hilo kwa mikono miwili. Mzee Marwa Mwita, akitoa tamko kwa niaba ya wazee wenzake, amesisitiza kuwa wamepokea maombi hayo ya Mkuu wa Wilaya kwa moyo wote na kuhakikisha kuwa katika eneo hilo hakuna mtu au kikundi kitakachojihusisha na vitendo hivyo vya kikatili, huku akionya kuwa watachukua hatua kali za kisheria na kijamii kwa yeyote atakayebainika kukiuka maagizo hayo.