Zoezi la makabidhiano ya ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mnazi Mmoja, Kata ya Mitengo, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, limekwama baada ya aliyepaswa kukabidhiwa ofisi hiyo kutofika katika eneo lililopangwa kufanyika kwa zoezi hilo Novemba 21, 2026.
Kukwama kwa zoezi hilo kumeibua sintofahamu kuhusu mustakabali wa uongozi wa mtaa huo, huku baadhi ya wananchi waliojitokeza wakieleza kutokubaliana na uamuzi wa kuondolewa kwa mwenyekiti wa mtaa huo, Saidi Mpondomoka, baada ya kupoteza sifa ya kuwa mwanachama wa CCM kufuatia kufukuzwa chamani.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Mpondomoka amesema kwa kuwa aliyepaswa kukabidhiwa ofisi hakufika, ataendelea kuitumikia nafasi hiyo hadi pale utaratibu mwingine utakapotangazwa. Ameongeza kuwa hadi sasa amepokea barua tatu kutoka CCM ngazi ya wilaya na mkoa zinazomtaka kuachia nafasi hiyo.
Aidha, Mpondomoka amewatoa hofu wananchi akieleza kuwa ataendelea kuwahudumia kwa kuwa bado anazo nyaraka za Serikali ya Mtaa wa Mnazi Mmoja hadi pale uamuzi mwingine utakapotangazwa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mitengo, Henry Lupapa, amesema atawasilisha kwa mamlaka husika maoni na hoja zilizotolewa na wananchi, huku akiwataka kuondoka katika eneo la ofisi hiyo. Hata hivyo, kukwama kwa makabidhiano hayo kunaacha sintofahamu kuhusu lini na kwa utaratibu gani mabadiliko ya uongozi wa mtaa huo yatatekelezwa.