Latest Posts

AFRIKA MTEGONI, HATARI YA KUTOKEA VITA KUU YA TATU YA DUNIA (WWIII)

Na mwandishi wetu,

Bila shaka wengi wetu hapa Duniani tumewahi kusikia au kusoma, kwa sababu sina hakika kama kwa sasa tunaweza kupata watu walioona moja kwa moja au kushiriki, ila kusikia na kusoma hiyo nina uhakika wa asilimia zote, hapa nazungumzia kuhusu uwepo wa ‘Vita Kuu ya Dunia’

‘Vita Kuu ya Dunia’ ni jina linalotumika kwa ajili ya vita inayohusu nchi/ mataifa mengi katika sehemu mbalimbali Duniani badala ya eneo la nchi kadhaa pekee kama ilivyokuwa kwa vita nyingi ambazo zimeshuhudiwa na nyingine zinaendelea kushuhudiwa hadi sasa hapa Duniani

Kama ambavyo tunafahamu kupitia kusoma au kusikia na masikioni mwetu ni jambo la kawaida kuhusu vita mbili kuu za Dunia zilizopigwa mnamo karne ya 20 ambazo kwa kawaida zinafahamika kwa majina ya ‘Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia’ iliyotokea kati ya mwaka 1914 hadi 1918 na ‘Vita Kuu ya Pili ya Dunia’ iloyoshuhudiwa kati ya mwaka 1939 hadi 1945

Kama nilivyoeleza hapo awali jina la ‘Vita Kuu ya Dunia’ limepatikana tangu mwanzo wa karne ya 20, na hiyo ilikuwa kabla hata ya ‘Vita Kuu ya Kwanza’ na hiyo ilikuja kutokana na ukweli kwamba endapo vita ikianzishwa na ikahusu sehemu kubwa ya Dunia ni lazima ipewe jina, na mawazo hayo yalikuja kutokana na mapatano dhaifu yaliyokuwepo wakati huo kati ya mataifa makubwa ya Ulaya ambayo mengi kama sio yote yalitawala nchi nyingi Duniani chini ya mfumo wa ukoloni

Wataalamu wa masuala ya historia wanadai kwamba hali halisi ya ‘Vita kuu ya Kwanza’ iliyohusisha mataifa mengi Duniani ilikuwa ni ile vita iliyodumu kwa kipindi cha miaka saba kuanzia 1756 hadi 1763 iliyohusisha Uingereza na madola ya Kijerumani, Uprusi na Hannover dhidi ya Ufaransa, Urusi, Austria, Uswidi, Saksonia na Hispania

Inadaiwa kuwa, mapigano hayo yaligusa maeneo mengi ya Ulaya, Amerika ya Kaskazini, Visiwa vya Karibi, India, Asia ya Mashariki, Afrika na Baharini kote Duniani, lakini ikumbukwe kuwa vita hii ilitokea kabla ya kupatikana kwa jina la ‘Vita Kuu ya Dunia’

Hata hivyo, kama nilivyoeleza hapo awali kupitia rekodi, na kumbukumbu mbalimbali ushuhuda mwingi kama sio wote unatambua vita vilivyotokea kati ya mwaka 1914 hadi 1918 kuwa ndio vinavyostahili kuitwa ‘Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia’, hilo liko hivyo, na litabaki hivyo haliwezi kubadilika

Sasa, vita hii iliitwa ‘Vita Kuu ya Dunia’ kwa sababu mapigano yake yalisambaa Duniani kote huku sehemu kubwa ya mapigano yalitokea maeneo ya Ulaya na Asia ya Magharibi, lakini pia katika makoloni ya Afrika, Asia na Pasifiki, kwa upande wa mataifa ya Amerika hayakuona mapigano kwenye nchi kavu lakini manowari za Ujerumani zilipigana na mataifa ya ushirikiano mbele ya pwani za Marekani na Amerika Kusini

Hii pia inaelezwa kuwa ilikuwa vita ya kwanza iliyopigwa Duniani ambayo habari zake ziliweza kufika katika muda wa masaa au siku chache kwa mataifa yote Duniani, na hiyo ni kutokana na upatikanaji wa vyombo vya mawasiliano hasa simu za kimataifa na redio kwa wakati huo

Kwa upande wa ‘Vita Kuu ya Pili ya Dunia’, hii ilikuwa vita iliyodumu kuanzia mwaka 1939 hadi 1945 ikihusisha kwa kiasi kikubwa mataifa ya Ujerumani, Italia, Japani na mataifa washirika wao kama vile Romania, Hungaria na Bulgaria dhidi ya nchi nyingi Duniani zilizoitwa mataifa ya ushirikiano hasa Uingereza, China, Urusi na Marekani

Dhamira ya makala yangu hapa si kujadili kuhusu uwepo wa jina la ‘Vita Kuu ya Dunia’ au kuingia ndani ya kutazama kuhusu zilivyokuwa ‘Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia’ na ‘Vita Kuu ya Pili ya Dunia’, la hasha, bila shaka hivi karibuni kama sio kuona, kusimuliwa au kusoma utakuwa umekutana na mjadala wa uwepo wa harufu ya kuwepo kwa ‘Vita Kuu ya Tatu ya Dunia (WWIII)’ na hapo ndipo kwenye msingi wa makala yangu leo

Miaka kadhaa iliyopita shirika la habari la kimataifa la Uingereza (BBC) kupitia machapisho, habari na makala zake kadhaa ilidai kuwa Dunia kwa sasa inakabiliwa na muongo hatari zaidi kuwahi kutokea katika maisha yote yaliyokuwepo hapa Duniani, ambapo tangu kumalizika kwa ‘Vita Kuu ya Pili ya Dunia’ haijawahi kushuhudiwa, na inaelezwa kuwa BBC walisema hayo kufuatia onyo lililokuwa limetolewa na Rais wa Urusi Vladimir Putin wakati huo

Katika mfululizo wa hotuba zake kipindi hicho Rais Putin alihalalisha uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, hatua ambayo imeiacha nchi yake ikitengwa jumuiya mbalimbali za kimataifa hadi sasa, ambapo katika hilo Rais Putin alizishutumu nchi za Magharibi kwa usaliti dhidi ya Urusi na kulazimisha washirika wake kuikacha Urusi jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limefanikiwa ukiacha mataifa machache tu yanayosimama na Urusi kwa sasa yakiwemo China na Korea Kaskazini

Siku moja, Rais Putin wakati akizungumza katika kongamano la kila mwaka la Valdai baada ya upinzani mkali wa kijeshi Ukraine aliweka wazi kuhusu hasira zake na za umma wa Urusi kutokana na harakati za kuwakusanya Warusi wapatao 300,000 kwa ajili ya kuongeza askari kusaidia vita

Siku moja kabla ya hotuba hiyo aliyoitoa huko jijini Moscow, alikuwa ameongoza mazoezi ya kawaida ya nyuklia ambayo yalihusisha shambulio la nyuklia la kukabiliana na shambulio kubwa la nyuklia la adui ambapo baada ya zoezi hilo alinukuliwa akisema, “hatujawahi kusema lolote kuhusu uwezekano wa Urusi kutumia silaha za nyuklia, tumejibu tu kwa vidokezo kwa maoni yaliyotolewa na viongozi wa nchi za Magharibi”

Kauli yake iliibua hisia mseto kutoka kila pembe ya Dunia huku wengi wao na hasa mataifa makubwa na yenye nguvu za kijeshi na kiuchumi kama vile Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na mataifa yote yaliyoko kwenye Jumuiya za NATO na Umoja wa Ulaya (EU) yaliendelea kuongeza wigo wa kuikumbatia Ukraine jambo ambalo limekuwa likileta minong’ono ya kuibuka kwa ‘Vita Kuu ya Tatu ya Dunia (WWIII)’

Kila uchwao na hususani siku za hivi karibuni kumekuwa na fukuto kubwa linalochomoza kuhusiana na hatari ya uwepo wa ‘Vita vya Tatu vya Dunia’, uwepo wa mashaka na wasiwasi huo ndio uliopelekea kufuatilia jambo hili kwa karibu sana ili nipate ABC na kwa kudonoadonoa nimeambulia machache kama ifuatavyo:-

Septemba 24 mwaka huu Dunia ilikaribia kushuhudia mabadiliko makubwa katika historia yake, Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer walikutana kujadili suala nyeti, na kwa pamoja walikubaliana kutoa ruhusa kwa Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi, hatua hii ilizua wasiwasi mkubwa wa kuibuka kwa vita vya moja kwa moja kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi

Ikumbukwe kuwa huko nyuma Rais Putin alishawahi kusema wazi kuwa mashambulizi ya makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi yangetafsiriwa kama hatua ya vita si kwa Ukraine pekee bali kwa Uingereza na Marekani pia, ambapo kwa mujibu wa Russian Military Doctrine imeeleza kuwa majibizano hayo ya nyuklia yanaweza kudumu kwa dakika 72 tu, ambapo ndani ya muda huo mfupi wa siku zisizozidi tatu tunaweza kushuhudia kusambaratika kwa mabara haya mawili ya Ulaya na Amerika Kaskazini na kuanzisha enzi ya maangamizi mapya Duniani

Nimepitia mijadala hii kwa karibu katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii na kwa upande wa X ambao zamani ulikkuwa ukifahamika kama Twitter nimekutana pia na uchambuzi wa UNITE @ifafricaute ambapo katika uchambuzi wake anadai kuwa makubaliano hayo hayakufikia mwisho, na hali haikutulia kama ilivyotarajiwa, lakini Marekani iliendelea kutoa msaada mkubwa kwa Ukraine ikiwa ni pamoja na silaha nzito na za kisasa, hatua iliyoongeza mvutano kati ya mataifa hayo makubwa

Ameendelea kufafanua kuwa katika wiki chache alizobakiza kuwepo ofisini kama Rais, Rais Biden wa Marekani amechukua uamuzi wa kukubaliana na ombi la Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya maeneo muhimu ndani ya Urusi ambapo hadi sasa inadaiwa kuwa Ukraine imeshatuma makombora kadhaa ya Marekani ndani ya Urusi

Hivyo, katika hali ya kukabiliana na mashambulizi ya kijeshi kutoka kwa Ukraine kwa msaada wa Marekani, Rais Putin amesaini hati mpya ya Russian Nuclear Doctrine ambayo inasema kwamba, ‘agression’ dhidi ya Urusi kutoka kwa nchi zisizo na silaha za nyuklia, lakini kwa msaada wa nchi inayomiliki silaha za nyuklia itachukuliwa kama shambulio la pamoja dhidi ya Urusi

Kama hiyo haitoshi, UNITE @ifafricaute anasema hatua hii ni majibu ya moja kwa moja kwa uamuzi wa Rais Biden kuruhusu matumizi ya makombora ya masafa marefu ya Marekani kama vile Attackums, kwa Ukraine katika vita dhidi ya Urusi

Katika jibu lake, Kremlin lilisema kuwa litachukulia mashambulizi ya kijeshi kutoka kwa Ukraine yaliyosababishwa na Marekani kama tishio la moja kwa moja kwa usalama wa Taifa, na kwamba Urusi haitaona haja ya kusita kutumia silaha za nyuklia ikiwa itashambuliwa kwa makombora ya kawaida, hasa yale yanayokuja kutoka kwa mataifa yenye uwezo wa nyuklia

Kwa upande waka, Marekani imesema kwamba licha ya tishio la Urusi kutumia silaha za nyuklia lakini hakukuwa na dalili za maandalizi ya haraka kutoka kwa Urusi ya kutumia silaha hizo, ingawa maoni kutoka kwa viongozi wa usalama wa Urusi yalikuwa wazi kuwa matumizi ya silaha za nyuklia ni mojawapo ya hatua zinazoweza kuchukuliwa iwapo mashambulizi hayo yataendelea, na Urusi hawezi kubali kushambuliwa bila kujibu kwa nguvu kubwa

Kwa upande wa Ulaya, inadaiwa kuwa baadhi ya nchi kama Italia zilijitenga na uamuzi wa Marekani huku Waziri Mkuu wa Italia Meloni akisema kuwa nchi yake haikubaliani na hatua ya Marekani ya kuruhusu mashambulizi ndani ya Urusi, hii inaonyesha mgawanyiko mkubwa ndani ya jumuiya ya kimataifa kuhusu jinsi ya kushughulikia mgogoro huo mkubwa wa kijeshi unaoendelea sasa Duniani

Kufuatia sintofahamu hiyo, hali ya wasiwasi imekuwa kubwa zaidi huku Dunia ikiangalia kwa makini kama hatua hii itazidisha mivutano na kuleta madhara zaidi kwa usalama wa kimataifa, au kama itakuwa njia ya kumaliza vita kwa kuonyesha msimamo thabiti dhidi ya Urusi

Inaelezwa kuwa baadhi ya wananchi wa Marekani wanaendelea kumuandikia Rais Putin barua za wazi kupitia majukwaa mbalimbali ya  mitandao wa kijamii ikiwemo X, wakisema, ‘Dear Putin please don’t let Biden start WW3’, ambapo kwa kiasi kikubwa wananchi hawa wanalaani uamuzi wa utawala wa Rais Biden kuruhusu Ukraine kutumia makombora ya ATACMS ya Marekani kushambulia Urusi, wakionesha wasiwasi mkubwa kuhusu hatari ya vita vikubwa iliyoko mbeleni

Lakini swali la kujiuliza hapa, je ni nini madhara ya vita hivi kwa Bara la Afrika endapo vikitokea

Kwa mara nyingine tena nimerejea kuangaza uchambuzi wa UNITE @ifafricaute ambaye anadai kuwa kwanza kabisa Bara la Afrika litakumbwa na ongezeko kubwa la bei za bidhaa muhimu kama mafuta na chakula, hali hiyo itatokana na usumbufu wa usambazaji wa bidhaa hizo Duniani huku mataifa makubwa yakijikita kwenye vita, kwa bara ambalo tayari lina changamoto za kiuchumi gharama hizi zitakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi wa kawaida

Pili, uwekezaji na misaada ya kimataifa inaweza kupungua kwa kasi kwani mataifa yanayosaidia Afrika yatakuwa yakitumia rasilimali zao kwa ajili ya vita, hii inaweza kuathiri maendeleo ya miradi mingi muhimu Barani Afrika kuanzia sekta za afya hadi elimu, isitoshe kuna hatari ya mataifa ya Afrika kujikuta yakihusishwa moja kwa moja kwenye mgogoro huu, iwe kwa njia ya kuchagua upande wa kushirikiana au hata kushinikizwa kuunga mkono mataifa fulani, hali inayoweza kusababisha migawanyiko ya kisiasa na hata kuathiri amani ya ndani ya nchi

Zaidi ya yote, vita vya Dunia vina uwezo wa kuibua wimbi jipya la wakimbizi na ukosefu wa usalama Duniani, Afrika kama ilivyo kwenye migogoro mingine ya kimataifa inaweza kubeba mzigo wa wakimbizi na changamoto zake na hapo ndipo tatizo linapoweza kuanza kutokea

Kwa kiasi kikubwa na kwa vyovyote itakavyokuwa kama mambo yatabaki kama ilivyo sasa huenda kukashuhudiwa uwepo wa ‘Vita Kuu ya Tatu ya Dunia (WWIII)’

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!