Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema utu wa taifa hupimwa kwa namna linavyowajali wazee wake, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma na mazingira yanayowezesha wazee kuishi kwa heshima, usalama na ustawi.
Mahundi ameyasema hayo alipofanya ziara katika Makazi ya Wazee na Wasiojiweza Kiilima yaliyopo Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, ambapo alikagua hali ya utoaji wa huduma, kusikiliza changamoto zinazowakabili wazee pamoja na kuhimiza maboresho ya ustawi wao.

Amesema Serikali imejipanga kuendelea kuboresha huduma za ustawi wa jamii kwa wazee kwa kuhakikisha wanapata huduma muhimu zikiwemo afya, lishe, malazi na huduma za kijamii nakueleza kuwa wazee ni hazina ya taifa kutokana na mchango wao katika ujenzi wa nchi, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuwalinda na kuwahudumia kwa stahiki.
”Hakuna jamii inayoweza kujivunia maendeleo ikiwa haiwajali wazee wake. Wizara inaendelea kutekeleza maboresho mbalimbali ya makazi ya wazee nchini kupitia uboreshaji wa miundombinu na huduma muhimu, wazee ni hazina ya Taifa letu, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha wanapata huduma stahiki na wanaishi katika mazingira salama na yenye heshima,” amesema Mahundi.

Awali, Afisa Mfawidhi wa Makazi ya Wazee na Wasiojiweza Kiilima, Gladness Rwiza, amesema kituo hicho ni miongoni mwa makazi 13 yanayomilikiwa na Serikali kupitia Wizara, nakuongeza kuwa kwa sasa makazi hayo yanawahudumia wazee 17, wakiwemo wanaume 13 na wanawake wanne.
Rwiza amesema makazi hayo yanatoa huduma mbalimbali ikiwemo malazi, chakula, matibabu, mavazi, ushauri nasaha, huduma za kiroho na ulinzi, huku pia yakitekeleza miradi ya maendeleo inayochangia ustawi wa kituo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amesema serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana na Wizara kuhakikisha Makazi ya Wazee Kiilima yanapata huduma zote muhimu kwa wakati, ikiwemo huduma za afya, ulinzi na mazingira bora ya kuishi.
