Shaban Moshi Shaban, Afisa usafirishaji kwa kutumia Pikipiki maarufu kama Bodaboda kwenye eneo la Kimara mwisho Mkoani Dar Es Salaam, ameishukuru serikali pamoja Vyombo vya ulinzi na usalama nchini Tanzania, kwa jitihada kubwa zilizochukuliwa ili kuirejesha amani ya Tanzania, akieleza kuwa vurugu za Oktoba 29, 2025 ziliwaweka kwenye wakati mgumu kiuchumi na kijamii.
Bw. Moshi wakati akizungumza na chombo hiki cha habari, amesema ghasia hizo pamoja na zuio la kutoonekana nje kuanzia saa kumi na mbili Jioni lililotolewa na Jeshi la Polisi liliwaletea athari nyingi za kiuchumi kutokana na kukosa abiria na kipato, kwani shughuli za usafirishaji walikuwa wamezoea kuzifanya kwa muda wa saa 24.
“Kitu walichokifanya waliokuwa wakijiita waandamanaji ni kitu ambacho hakifai kwani maandamano haya hayakuwa na ujumbe wowote kwa serikali lakini pia maandamano yale yalikuwa kosa kisheria kwasababu walifanya uhalifu pia katika baadhi ya sehemu kwahiyo niwashauri waache hicho walichokifanya.” Amesema Bw. Moshi.
Aidha ameeleza pia namna ambavyo mfumuko wa bei uliwaathiri kwa kiasi kikubwa, akisema mafuta ya petroli yaliuzwa kwa shilingi 15,000 kwa Lita moja hivyo kusababisha adha kubwa kwao ikiwa ni pamoja na kuwapoteza wateja waliolalamikia kupanda kwa bei za usafiri huo wa Pikipiki.