Siku chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 nchini, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt. Benson Bagonza ameibuka na tafakuri kuhusiana na ushindi wa kishindo ilioupata chama tawala CCM katika uchaguzi huo
Kupitia tafakuri hiyo Askofu Dkt. Bagonza amehoji endapo ushindi huo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni ‘ushindi wa kishindo’ au ‘kishindo cha ushindi’ akitumia nadhamira ya kupatikana kwa asilimia 99 kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 huku akirejea matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo chama hicho tawala pia kiliibuka kidedea kwa kishindo kama hicho kwenye nafasi za Bunge, huku pia ikipata kishindo kwenye kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na hata viti vya Udiwani
Kupitia tafakuri hiyo, Askofu Dkt. Bagonza ni kama vile ‘ametilia shaka’ ushindi huo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) huku mashaka yake kwa kiasi kikubwa yakionekana kwa namna ambavyo inawezekana matokeo hayo yakapunguza au kudhoofisha uwajibikaji wa serikali kutokana na kile kinachoonekana kwamba idadi kubwa ya vyombo vya maamuzi ikiwemo Bunge, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Halmashauri na serikali za mitaa zote zina wawakilishi wa chama kimoja tawala kwa asilimia 99, kupitia tafakuri hiyo Askofu Dkt. Bagonza ameandika yafuatayo:-
“Tumemaliza uchaguzi walioshinda wamepata asilimia 99.99 (serikali za mitaa) na Bunge letu bado ni asilimia 99, huu ni ushindi wa kishindo au kishindo cha ushindi?”
“Tukubaliane; tuna watu wengi ni waaminifu kwa sababu hawana cha kuiba au wanaogopa kukamatwa, kama wangepata cha kuiba na wakawa hawana wasimamizi wangeiba tu, uaminifu haupimwi kwa kutoiba tu bali kwa kuwa na cha kuiba lakini ukashinda jaribu la kuiba, serikali nyingi ziko hivyo zinahitaji kusimamiwa, kuchunguzwa, kukosolewa ili zifanye vizuri, hata katika ‘Ulimwengu wa Imani’, uwepo wa shetani ni msingi wa jitihada za kufundisha uadilifu”
“Marekani wamemaliza uchaguzi wao, Urais umeenda kwa chama cha Republican kilichokuwa chama cha upinzani kabla ya uchaguzi, licha ya kumpata Rais pia kimepata viti 53 dhidi ya 47 vya Democrats, Bungeni (Congress) Republican wana viti 220 na Democrats wana viti 214”
“Kwa hiyo Rais mteule Donald Trump atakuwa Ikulu bila kuwa na wingi wa kutisha wa Wabunge na kwenye Senate, Democrats ndio walikuwa chama tawala kabla ya uchaguzi, hali hii inaweza kubadilika baada ya miaka miwili utakapofanyika uchaguzi mdogo (nusu muhula) kwa baadhi ya majimbo ya Bunge na Senate, kwenye uchaguzi huo Trump anaweza kukosa wingi kwenye Bunge na Senate, kwa nini?”:-
(i) Wamarekani hawapendi kuweka mayai yote kikapu kimoja (Urais, Ubunge na Useneta), ukipewa Urais unanyimwa ama Wabunge au Maseneta ili ujifunze kushirikiana na wapinzani kwa kutumia hoja siyo bunduki,
(ii) Check and balance (kuwajibishana) ni msingi wa maamuzi ya kila kitu, hata kwenye vyombo vya habari ni lazima kikisemwa kitu sharti upande wa pili uwekwe ili wasomaji/ wasililizaji wajue pande mbili na kuamua wenyewe,
“Kimantiki, ushindi wa kishindo chaweza kuwa chanzo cha mdororo wa maendeleo katika bara letu (Afrika) linalopenda sana neno ‘ndiyo’, tabia ya kuchukia maoni tofauti inadumaza utundu, ugunduzi, na ubunifu, badala yake dhana ya ‘ndiyo’ inakomaza kukariri, woga, utii usio na dhamiri na kuondoa uendelevu (sustainability) katika maamuzi mengi, mfumo wa elimu ndilo jiko la kupika Taifa linalohoji ‘kwa nini?’ au Taifa linaloimba ‘ndiyo’ kwa kila kitu”
“Mfungwa katika gereza la ‘ndiyo’ akiwekewa mkate na funguo za gereza akaambiwa achague moja, atachagua mkate, mfungwa katika gereza la ‘kwa nini’ akiwekewa hivyo viwili anaweza akahoji kwa nini si vitatu badala ya kuchagua kama alivyoelekezwa”
“Zawadi ya mfungwa ni uhuru si sabuni ya kuoga akiwa gerezani, kumwachia huru mfungwa ni sawa na kumweka huru Askari magereza anayemlinda, hiyo ndiyo faida kuu ya uhuru unanufaisha pande zote, ushindi wa kishindo ni kujipiga risasi mguu, wenzako wakikosa mtu wa kuwapinga, wanageuka kuwa wapinzani wako”