Latest Posts

CARE INTERNATIONAL NA MWANAMKE INITIATIVES FOUNDATION WAZINDUA MPANGO WA KUWAANDAA VIONGOZI WANAWAKE VIJANA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa jamii kuwapa wanawake nafasi na sauti katika uongozi, akisema kuwa bila juhudi za makusudi za kuwaunga mkono, usawa wa kijinsia hautafikiwa.

Waziri Gwajima ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam, Februari 11, 2025 alipohutubia kama mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa Programu ya Uongozi wa Wanawake Vijana (Young Women Leadership Program – WYLP).

“Tunahitaji kuwa mstari wa mbele kuwasemea viongozi wanawake na kuwahamasisha kushiriki kwenye nafasi za uamuzi. Usipowasemea viongozi wanawake, nasi hatutasemewa. Lazima tuelewe kuwa maendeleo ya jamii yoyote yanategemea ushiriki wa jinsia zote,” amesema Dkt. Gwajima

Akieleza umuhimu wa mpango huo, amefafanua kuwa WYLP, unaoratibiwa na Care International Tanzania kwa kushirikiana na Mwanamke Initiatives Foundation, umelenga kuwaandaa wanawake vijana wenye umri wa miaka 20-35 kushika nafasi za uongozi katika sekta mbalimbali.

Dkt. Gwajima amebainisha kuwa, licha ya mafanikio fulani, wanawake bado wanakumbana na changamoto nyingi katika kushika nafasi za uongozi.

“Bungeni tunao wanawake takribani asilimia 36-37, lakini katika ngazi nyingine za maamuzi, hususan sekta binafsi, idadi hiyo ni ndogo mno. Asilimia 20 tu ya wanawake wako kwenye nafasi za juu kama wakurugenzi au wajumbe wa bodi. Lazima tubadili hii hali,” amesisitiza.

Ameitaka jamii kuondoa vikwazo vya kimfumo, kiutamaduni na kifikra vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na kufanya maamuzi yanayoathiri maendeleo ya taifa.

Naye, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesisitiza kuwa wanawake wamekuwa viongozi wa asili kupitia majukumu yao katika familia na jamii, huku akiwataka wanawake vijana kutumia fursa kama WYLP kujiandaa kwa nafasi za uongozi na kushirikiana kuleta mabadiliko ya kweli.

“Katika familia, mama ndiye kiongozi wa kwanza wa mtoto. Ikiwa wanawake wanaweza kulea familia na kuongoza majukumu ya nyumbani, basi wana uwezo wa kuongoza pia serikalini, katika biashara na sekta nyinginezo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Care International Tanzania, Prudence Masako, amesema kuwa shirika lake limekuwa likifanya kazi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, lakini limebaini kuwa bado kuna pengo kubwa katika nafasi za uongozi.

“Tumefanikiwa kuwawezesha wanawake wengi kiuchumi, lakini bado wengi wao hawapo kwenye maamuzi makubwa. Kupitia WYLP, tunataka kuhakikisha kuwa wanawake wanakuwa sehemu ya viongozi wa kesho,” amesema.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Mwanamke Initiatives Foundation, Wanu Hafidh, ameeleza kuwa yeye mwenyewe ni mnufaika wa programu za uongozi na anafahamu umuhimu wake kwa wanawake vijana, hivyo anaamini kuwa programu hiyo itatoa mafunzo ya uongozi, ushawishi na utetezi wa haki za wanawake, hivyo kuwawezesha wanawake vijana kushika nafasi mbalimbali za maamuzi.

“Baada ya kuhitimu mafunzo kama haya, hatua inayofuata ni utekelezaji wa yale tuliyojifunza ili kuleta mabadiliko. Uzinduzi wa WYLP ni sehemu ya kuandaa viongozi wa baadaye ambao watakuwa na mchango mkubwa katika jamii na taifa kwa ujumla,” amesema.

Miongoni mwa wanufaika wa programu hiyo, Jennifer Shigholi, amesema kuwa mafunzo aliyopata kupitia WYLP yamemwezesha kuboresha ujuzi wake wa uongozi na uchechemuzi katika sekta ya kilimo cha mwani Zanzibar.

“Nimepata ujasiri wa kuzungumza na kufanya maamuzi muhimu. Natamani kuona wanawake wengi zaidi wakitumia fursa hii kujiendeleza,” alisema.

Amewataka wanawake vijana kuungana na kushirikiana katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya jamii nzima.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!