Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Makete mkoani Njombe kimewaonya wanaoingilia mamlaka na kuweka wazi mitandaoni majina ya wagombea wakidai yamekatwa na kuwataka kuacha utaratibu wa chama ufanye kazi.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete, Clement Ngajilo ametoa onyo hilo wakati akizungumza kwenye kikao cha wadau wa maji Makete kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi za halmashauri hiyo.
“Kwenye mitandao watu wanatoa taarifa ambazo sio sahihi na zinaleta taharuki kwamba mara huyu kakatwa, wameingilia mamlaka ambayo siyo ya kwao, Chama hiki kimeweka utaratibu, kuanzia tarehe 18 au 19 mtapata taarifa”, amesema Ngajilo.
Amewataka wagombea ambao majina yao hayatarudi kuwa watulivu na kutonuna kwa kuwa watabaki kuwa akiba ya chama.
“Majina ambayo yatakuwa hayajarudi wewe unabaki kuwa akiba ya chama usinune nafasi ni tatu, na tutaungana na wale watatu tumpate mmoja anayekubarika na jamii sio na watu wachache”, amesema Ngajilo.