Latest Posts

CHADEMA MBEYA YAAPA KUIONDOA CCM MADARAKANI 2024/2025

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya kimewataka wananchi kwenda kuichagua CHADEMA kwenye uchaguzi ujao ili kuwaletea maendeleo ya kweli badala ya kuendelea kufumbia macho kile ilichoita vitendo vya ufujaji fedha za umma na maisha ya wananchi kuendelea kuwa magumu.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya Masaga Pius Kaloli wakati akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Utengule Usongwe.

Masaga amesema CHADEMA ni chama chenye sera nzuri tofauti na CCM ambayo zaidi ya miaka sitini imekuwa ikihubiri maendeleo lakini hayaonekani kutokana na baadhi ya kero kuendelea kulikabili Taifa tangu uhuru.

Mwenyekiti huyo anasema uchaguzi ujao ni vema wananchi wakachagua viongozi bora kwa maendeleo yao wenyewe akisema CHADEMA ndio itakuwa na wagombea imara.

Naye mwenyekiti wa chama hicho jimbo la Mbeya vijijini Getruda Japhet Lengesela, amewataka wananchi kuendelea kuiamini CHADEMA akisema ndicho chama kilichobeba maono ya kweli katika kuwatumikia wananchi.

Getruda anasema pamoja na uchaguzi mkuu, pia kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa CHADEMA imejipanga kusimamisha wagombea katika vitongoji na vijiji vyote na watahakikisha wanashinda huku akiwataka wanawake kutojidharau badala yake wajitokeze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Mwenyekiti wa Baraza la wazee mkoa wa Mbeya David John Mwambigija amesikika akisema CHADEMA ndiyo safina iliyobeba matumaini ya wananchi na wanaoendelea kuipenda au kuishabikia CCM ni kukosa maono ya maendeleo endelevu.

Huu ni mwendelezo wa mikutano ya CHADEMA mkoani Mbeya kukagua uhai wa chama na kutoa elimu ya uraia kwa wananchi huku pia chama hicho kikiendelea kunadi sera zake ili kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi kwenye chaguzi zijazo kikibeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM kuwa haina jipya lililofanyika badala yake tumaini la kweli ni CHADEMA.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!