Latest Posts

CHAUMMA BUKOBA MJINI YAPANIA KULETA MADILIKO CHANYA KATIKA UJENZI WA MAENDELEO

Theophilida Felician Kagera.

Mgombea ubunge wa Bukoba Mjini kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Bw. Saulo Joseph Kamugisha, ameweka bayana mpango wa chama hicho katika kuwaletea wananchi mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo endapo atapewa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Akizungumza mjini Bukoba, Saulo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Tumaini Jema, alisema dhamira yake ni kusukuma kasi ya maendeleo kwa vitendo na si kwa maneno pekee, akibainisha kuwa Bukoba inapaswa kusonga mbele kupitia matumizi ya fursa zilizopo.

“Natamani kuona Bukoba inabadilika kimaendeleo. Nitawajibika ipasavyo kwa hoja zenye tija na vitendo halisi. Mkoa wetu wa Kagera una fursa nyingi—kuanzia Ziwa Victoria hadi mipaka na nchi jirani—ambazo zikibuniwa vizuri zitainua uchumi wa wananchi,” alisema Saulo.

 

Vipaumbele vya CHAUMMA

Mgombea huyo alitaja vipaumbele vya chama chake kuwa ni kuboresha uchumi, elimu, maji, afya, uvuvi, na miundombinu ya kijamii. Aidha, aliahidi kuhakikisha miradi ya kimkakati katika jimbo hilo, ikiwemo Soko Kuu la Bukoba na barabara zinazojengwa, inakamilika kwa wakati.

Akiwa na elimu ya Shahada ya Usimamizi wa Mazingira (SUA) na Shahada ya Uzamili ya Afya ya Jamii (MUHAS), pamoja na uzoefu wa kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia mashirika ya World Vision na Tumaini Jema, Saulo aliomba wananchi kumchagua kwa kishindo ili awe mwakilishi wa kweli wa maendeleo.

Kwa upande wake, Katibu wa CHAUMMA Mkoa wa Kagera na Mwenyekiti wa Jimbo la Bukoba Mjini, Prosper Mbakile, alisema chama hicho kimejipanga ipasavyo kwa kusimamisha wagombea imara katika maeneo mbalimbali ya mkoa.

“CHAUMMA imewateua madiwani na wabunge wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi. Tuna wagombea katika majimbo ya Ngara, Biharamulo, Muleba Kusini na Bukoba Vijijini. Tunaamini wananchi wakituunga mkono tutaleta mageuzi,” alisema Mbakile.

Aidha, aliwataka wagombea wa chama hicho kufanya siasa safi zenye kujenga hoja badala ya kushambuliana au kubeza, akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji mijadala yenye mashiko na si matusi majukwaani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!